Russia: Chaguo la kijeshi halitasaidia kutatuliwa mgogoro nchini Yemen
Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, chaguo la kijeshi haliwezi kusaidia katika kutatua mgogoro wa Yemen.
Vasily Nebenzya, ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichochunguza matukio ya Yemen na kubainisha kwamba, ili kutatuliwa mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu kunahitajika njia ya kisiasa na kwa pande zote kuwa na mtazamo mmoja kwamba chaguo la kijeshi haliwezi kusaidia katika kutatuliwa mzozo wa nchi hiyo. Vasily Nebenzya amesisitiza kwamba, Russia inakaribisha na kuunga mkono mwito wa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen wa kuitishwa kikao cha mazungumzo kati ya pande za Yemen, kitakachofanyika mwezi Septemba mwaka huu.
Jana usiku Martin Griffiths, mjumbe maalumu wa UN katika masuala ya Yemen alitangaza kwamba tarehe sita mwezi ujao, mji wa Geneva, Uswisi, utakuwa mwenyeji wa duru mpya ya mazungumzo kati ya pande zinazohasimiana nchini Yemen. Aidha aliongeza kwamba, uthabiti na usalama wa bandari ya Al Hudaydah lazima uhifadhiwe, kwa kuwa bandari hiyo ni yenye umuhimu wa kipekee kwa ajili ya utumaji wa misaada ya kibinaadamu nchini humo.