Trump azidi kusakamwa, Russia nayo yaongeza ushuru wa bidhaa za Marekani
Serikali ya Russia imezipandishia ushuru bidhaa za Marekani ikiwa ni kujibu hatua ya rais wa nchi hiyo, Donald Trump ya kuzipandishia ushuru bidhaa ya chuma cha pua na aluminium zinazoingizwa nchini Marekani kutokea Russia.
Kuanzia jana Jumapili, serikali ya Russia imeweka ushuru mpya kwa bidhaa za Marekani zinazoingia nchini humo kama vile magari mazito ya kutengenezea barabara, zana za uchimbaji wa mafuta na gesi na vifaa vya uchimbaji wa chuma cha pua na kupasua majabali makubwa. Ushuru huo mpya uliotangazwa Russia kwa bidhaa za Marekani unaonesha ongezeka la asilimia 25 hadi 40 la ushuru.
Kabla ya hapo, Maxim Oreshkin, waziri wa ustawi wa kiuchumi wa Russia alikuwa ametangaza kwamba, ushuru mpya utakaowekwa na Russia kwa bidhaa za Marekani utakuwa ni sawa na dola milioni 87.6 kwa mwaka na kwamba Moscow ina haki ya kufanya hivyo kwa mujibu wa usuli na sheria za Shirika la Biashara Ulimwenguni.
Itakumbukwa kuwa tarehe 22 Juni 2018, serikali ya Donald Trump wa Marekani iliziongezea ushuru kwa asilimia 25 bidhaa za feleji na chuma cha pua za Russia na asilimia 10 ya ushuru zikawekewa bidhaa za aluminium za nchi hiyo zinazoingia nchini Marekani. Nyongeza hiyo ya ushuru imezikumba nchi kadhaa kama vile Russia, India, China, Canada na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Nchi mbalimbali zinaendelea kuongeza ushuru wa bidhaa za Marekani zinazoingia katika nchi hizo kama sehemu ya kujibu siasa hizo za kibeberu za Trump.