Nchi za Ulaya zapinga vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran
Nchi za Ulaya zimetangaza kupinga vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kutangaza kuunga mkono mapatano ya nyuklia maarufu kama JCPOA.
Katika taarifa kufuatia kurejeshwa vikwazo vya nyuklia vya Marekani dhidi ya Iran, Tume ya Umoja wa Ulaya imetoa taarifa na kutangaza kuendelea kuunga mkono mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji. Katika ujumbe kupitia Twitter, Tume ya Umoja wa Ulaya imesema sheria ya kukabiliana na vikwazo imefanyiwa marekebisho ili kuyafanya mashirika ya Ulaya yasidhuriwe na vikwazo vya Marekani.
Wakati huo huo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Alistair Burt amesema mashirika ya Ulaya yatalindwa ili yasidhurike kutokana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

Naye Msemaji wa Serikali ya Uingereza Edwin Samuel amesema nchi yake inaamini kuwa mapatano ya nyuklia ya Iran yanapaswa kulindwa.
Leo Jumanne Marekani imetangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran hatua ambayo inaendelea kukosolewa na nchi mbali mbali za dunia wakiwemo waitifaki wa Washington barani Ulaya.