Msimamo wa Russia kuhusu bajeti mpya ya jeshi ya Marekani
Bajeti ya masuala ya kijeshi isiyo na kifani ya dola bilioni 716 iliyosainiwa hivi karibuni na Rais Donald Trump wa Marekani imekabiliwa na radiamali kali katika upeo wa kimataifa.
Kwa kutilia maanani kwamba, katika stratejia yake mpya ya usalama wa taifa, Washington imeitaja waziwazi Russia kuwa ni adui na tishio kubwa kwa Marekani, Moscow inafuatilia kwa makini masuala ya kijeshi na kiusalama ya Marekani ikiwa ni pamoja na kupasishwa bajeti mpya ya jeshi la nchi hiyo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Russia, Maria Zakharova ameitaja bajeti mpya ya masuala ya kijeshi ya Marekani kuwa ni nembo ya ubeberu wa kijeshi wa serikali ya Washington duniani. Zakharova amesema: "Bajeti ya ulinzi wa taifa mwaka 2019 iliyotiwa saini na Rais Donald Trump wa Marekani ni kielelezo cha siasa za kibeberu za Washington katika upeo wa dunia."
Kimsingi Trump ameamua kutekeleza sera za kutumia nguvu za jeshi kwa shabaha ya kufikia malengo yake ya nje ya nchi. Sambamba na hayo siasa za kigeni za kiongozi huyo wa Marekani zinategemea sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na suala hili linairejesha Marekani katika kipindi cha utawala wa George W. Bush ambaye katika muongo wa kwanza wa karne hii ya 21 alizishambulia nchi za Afghanistan na Iraq kwa kisingizio cha mapambano ya dunia dhidi ya ugaidi. Hata hivyo sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Trump mbali na upande wake wa kijeshi na kiusalama unaodhihirika katika sura kujifanya polisi wa dunia na kutaka kuziburuta nchi nyingine, zinayo sura nyingine. Katika upande huo Marekani inatumia pia nguvu ya uchumi kwa kuziwekea vikwazo nchi mbalimbali. Sambamba na wenzo huo, nguvu za kijeshi na kutunisha misuli kwa ajili ya kuzitia woga na wahka nchi nyingine bado inapewa umuhimu na utawala wa sasa wa Marekani kwa ajili ya kutimiza malengo yake ya kigeni. Mfano wa ukweli huo ni mashambulizi ya makombora ya Marekani dhidi ya Syria na kutumwa manowari kadhaa zinazobeba makumi ya ndege za kivita kandokando ya Peninsula ya Korea kwa shabaha ya kuitisha na kuitia woga Korea Kaskazini.
Hii ni pamoja na kuwa ongezeko kubwa la bajeti ya masuala ya kijeshi ya Marekani linayanufaisha makampuni ya kutengeneza silaha ya nchi hiyo. Andrei Frolov ambaye ni mtaalamu wa Kituo cha Tathmini, Stratejia na Teknolojia cha Russia anasema: Mashirika na makampuni makubwa ya viwanda vya masuala ya kijeshi ya Marekani daima yamekuwa yakidhibitiwa na kusimamiwa na Warepublican, na sasa Donald Trump anataka kupata ridhaa yao kwa kutenga bajeti kubwa ya masuala ya kijeshi.
Wakati huo huo katika nyaraka zinazohusiana na masuala ya kijeshi na kiusalama ya Marekani kama stratejia ya usalama wa taifa, stratejia ya ulinzi wa taifa na ilani mpya ya silaha za nyuklia ya Marekani, daima Russia inatambuliwa kuwa ndio tishio kubwa zaidi la nchi hiyo na tishio nambari moja la silaha za nyuklia. Washington inaitambua Russia na baada yake China kuwa ni tishio kuu la usalama wake na hapana shaka kuwa kuzidishwa kwa bajeti ya jeshi la Marekani kunafanyika kwa shabaha ya kukabiliana na nchi hizo katika daraja ya kwanza. Vivyo hivyo kutengwa kwa bajeti kubwa ya kusasisha silaha za nyuklia na kuanzisha jeshi la anga za mbali huko Marekani kunafanyika kwa lengo la kukabiliana na kile kinachoitwa vitisho vya Moscow na Beijing.
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia, Sergei Ryabkov anasema: Moscow ina wasiwasi kuhusu bajeti isiyo na kifani iliyopasishwa na Marekani kwa malengo ya kijeshi, na inadurusu na kuchunguza kwa makini bajeti hiyo kabla ya kuchukua hatua yoyote kuhusu suala hilo.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, kupasishwa kwa bajeti mpya ya masuala ya kijeshi ya Marekani ni kielelezo cha kuendelezwa sera za White House za kufuatilia malengo ya Marekani kikanda na kimataifa kwa kutumia mabavu na nguvu za jeshi. Suala hilo linazusha wasiwasi mkubwa katika upeo wa kimataifa kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa na Marekani katika siku zijazo kwa ajili ya kuvuruga mfumo wa kimataifa.