Russia, China zasisitiza kulinda mapatano ya nyuklia ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i47518-russia_china_zasisitiza_kulinda_mapatano_ya_nyuklia_ya_iran
Russia na China zimesistiza kuwa zitaendelea kufungamana na mapatano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015 yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 18, 2018 02:48 UTC
  • Russia, China zasisitiza kulinda mapatano ya nyuklia ya Iran

Russia na China zimesistiza kuwa zitaendelea kufungamana na mapatano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015 yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA.

Aidha nchi hizo zimesisitiza kudumisha uhusiano na ushirikiano wao na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na vikwazo vipya vya Marekani. Katika taarifa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema nchi hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake katika mapatano ya nyuklia ya Iran.

Taarifa hiyo imesema Shirika la Nyuklia la Russia la Rosatom limeanzisha miradi kadhaa ya kuhakikisha kufungamna na mpango wa nyuklia wa Iran.

Siku ya Ijumaa pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alisisitiza kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Iran, Mohammad Javad Zarif, ameongeza kuwa mapatano ya JCPOA ni kwa mujibu wa maslahi ya pamoja ya jamii ya kimataifa.

Mnamo Mei 8, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa nchi yake inajiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaliyofikiwa baina ya Iran na madola sita makubwa duniani ambayo ni Marekani yenyewe, Uingereza, Ufaransa, Russia, China na Ujerumani.

Hatua hiyo ilipingwa vikali na nchi zingine katika mapatano hayo hasa Russia na China.