Uhispania yawapokea wakimbizi elfu kumi bila ya wazazi wao
Wizara ya Afya ya Uhispania imetangaza kuwa Madrid inakadiria kuwa wakimbizi 10,000 walio chini ya miaka 18 wapo katika ardhi ya Uhispania peke yao bila ya wazazi wao na imetenga yuro milioni 40 kwa miji ya nchi hiyo inayotaka kuwapokea wakimbizi hao.
Serikali ya Kisoshalisti ya Uhispania ambayo iko madarakani kwa miezi mitatu sasa imechukua hatua hii ya aina yake licha ya nchi hiyo kukabiliwa na wimbi kubwa la wakimbizi miezi kadhaa iliyopita. Wakimbizi 49 wasio na wazazi wao kutoka kaskazini mwa Afrika jana asubuhi waliwasili katika pwani ya mji wa Tarifa kusini mwa Uhispania kwa kutumia boti dhaifu.
Wizara ya Afya ya Uhispania imesema serikali imetenga bajeti ya yuro milioni 40 zitakazogawiwa katika mikoa ambayo itawakaribisha wakimbizi watoto wasio na wazazi kutoka nje. Carmen Monton Waziri wa Afya wa Uhispania amesema kuwa hivi sasa kuna wakimbizi elfu kumi wa aina hiyo nchini humo.
Mwezi Aprili mwaka huu serikali ya Kihafidhina ya wakati huo iliwasajili wakimbizi waliowasili nchini humo bila ya wazazi wao zaidi ya 6,200 kulinganisha na wakimbizi wa aina hiyo 4000 waliowasili nchini humo mwaka 2016.