Idadi ya waliopoteza maisha katika zilzala, tsunami Indonesia yapindukia 1,200
Idadi ya watu walioaga dunia kutokana na tsunami na mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokikumba kisiwa cha Sulawesi mashariki mwa kisiwa cha Borneo nchini Indonesia imeogezeka na kufikia watu 1,234.
Idara ya Kupambana na Majanga nchini humo imesema leo Jumanne kuwa, idadi hiyo imeongezeka kutoka 844 iliyotangazwa hapo awali, na kwamba inashirikiana na timu za waokoaji katika shughuli za kupekeu vifusi ili kuwasaka manusuru na wahanga zaidi ya majanga hayo.
Zilzala hiyo yenye ukubwa wa 7.5 kwa kipimo cha rishta, iliutikisa mji wa Palu katika kisiwa hicho siku ya Ijumaa na kusababisha mawimbi makubwa ya tsunami yaliyousomba mji huo.
Tayari watu zaidi ya 800 wameshazikwa katika makaburi ya umati kwa lengo la kuzuia uwezekano wa kusambaa magonjwa katika maeneo yaliyoathirika na majanga hayo ya kimaumbile.
Mwezi Agosti mwaka huu, watu 319 walipoteza maisha kutokana na tetemeko jingine la ardhi katika eneo la Lombok nchini Indonesia.
Inafaa kukumbusha hapa kuwa, mwaka 2004 zilzala ya chini ya maji ilitokea katika Bahari Hindi na kusababisha tsunami katika nchi kadhaa huku Indonesia ikiathiriwa zaidi. Watu 170,000 walifariki dunia kwenye janga hilo la kimaumbile nchini Indonesia hususan katika mkoa wa Aceh.