Russia yafichua njama ya magaidi ya kutumia silaha za kemikali Syria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i48769-russia_yafichua_njama_ya_magaidi_ya_kutumia_silaha_za_kemikali_syria
Russia imetangaza kuwa, ina habari za kipelelezi kuhusu njama inayopangwa na magaidi kwa ajili ya kutumia silaha za kemikali katika eneo la Idlib huko kaskazini magharibi mwa Syria.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 13, 2018 15:55 UTC
  • Russia yafichua njama ya magaidi ya kutumia silaha za kemikali Syria

Russia imetangaza kuwa, ina habari za kipelelezi kuhusu njama inayopangwa na magaidi kwa ajili ya kutumia silaha za kemikali katika eneo la Idlib huko kaskazini magharibi mwa Syria.

Mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) huko The Hague nchini Uholanzi, Alexander Shulgin amesema kuwa, Moscow ina taarifa za kiintelijensia zinazoonesha kuwa, makundi ya kigaidi katika eneo la Idlib yanapanga njama ya kutumia silaha za kemikali katika eneo hilo la kuisingizia serikali ya Damascus. 

Shulgin ameongeza kuwa, Russia imekutana na wanachama wa Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali na kuwakabidhi nyaraka hizo za kiintelijensia. 

Mwakilishi wa Russia katika shirika la OPCW amesema kuwa, wanachama wa kundi la White Helmets nchini Syria walifanya juhudi za kuzusha na kubuni urongo kuhusu utumiaji wa silaha za kemikali nchini Syria na kulibambikia jeshi la nchi hiyo ili kutayarisha mazingira ya kufanyika mashambulizi ya nchi za Magharibi dhidi ya nchi hiyo.

Wanachama wa makundi ya kigaidi Syria.

Mwezi Septemba mwaka huu msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia, Maria Zakharova alitangaza kuwa, kundi la kigaidi linalojiita Tahriru Sham na wanachama wa White Helmets wanapeleka mada ya gesi ya sarin katika eneo hilo kwa shabaha ya kuisingizia serikali ya Syria kwamba imeshambulia wakazi wake kwa silaha za kemikali. 

Marekani na washirika wake wa Magharibi wamekuwa wakitumia visingizio kama hivyo kwa ajili ya kufanya hujuma na mashambulizi dhidi ya maeneo ya jeshi la serikali ya Syria.