AI yailaumu Ufaransa kwa kuiuzia silaha serikali ya Misri
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty international limeikosoa vikali Ufaransa na nchi nyingine kadhaa za Ulaya kwa kuendelea kuiuzia silaha serikali ya Misri na kusema kwamba, zimekiuka maamuzi ya Umoja wa Ulaya ya kupiga marufuku kuiuzia silaha serikali ya Cairo.
Taarifa iliyotolewa na Amnesty International imesema kuwa, Paris imekiuka sheria za kimataifa kwa kuiuzia silaha serikali ya Misri katika kipindi cha baina ya mwaka 2012 na 2015 ambazo zimetumiwa kukandamiza waandamanaji dhidi ya serikali.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mwaka 2013 Umoja wa Ulaya ulizitaka nchi zote wanachama kusitisha mauzo ya silaha kwa serikali ya Misri lakini nchi kadhaa za bara hilo ikiwemo Ufaransa, Uhispania, Italia, Uingereza, Ujerumani na Romania zimepuuza marufuku hiyo.
Taarifa ya Amnesty international imesema mwaka 2013 Ufaransa iliongoza kwa kuwa muuzaji mkubwa zaidi wa aina mbalimbali za silaha kwa utawala wa Misri na kwamba ilizipita hata nchi kama Marekani.
Itakumbukwa kuwa mwaka huo huo wa 2013 jeshi la Misri liliiondoa madarakani serikali ya kwanza kuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia nchini humo.
Mwaka huo huo serikali ya Cairo ikiongozwa na Jenerali Abdul Fattah al Sisi aliyeongoza mapinduzi dhidi ya serikali halali ya nchi hiyo ilifanya mauaji dhidi ya melfu ya raia walikuwa katika maandamano na mgomo wa kuketi chini katika medani za Rabaa al-Adawiya na al-Nahda mjini Cairo.