IPU yapiga marufuku mijadala kuhusu ushoga na usagaji
(last modified Thu, 18 Oct 2018 15:29:20 GMT )
Oct 18, 2018 15:29 UTC
  • IPU yapiga marufuku mijadala kuhusu ushoga na usagaji

Kikao cha 139 cha Jumuiya ya Kimataifa ya Mabunge (IPU) kimepiga kura kuunga mkono hoja ya kutaka kupiga marufuku mijadala inayohusu masuala ya ushoga na usagaji.

Hoja hiyo imewasilishwa katika kikao cha IPU mjini Geneva nchini Uswisi na ujumbe wa Uganda ukiongozwa na Spika wa Bunge la nchi hiyo ya Afrika Mashariki, Bi. Rebecca Kadaga. 

Waliopiga kura kuunga mkono hoja ya kutojadiliwa ajenda ya uozo huo wa jamii wamesema wamelazimika kufanya hivyo baada ya wajumbe kutoka Canada na Ubelgiji kulobi wanachama wa jumuiya hiyo ya kimataifa ili waunge mkono mijadala ya kutetea eti haki za mashoga, wasagaji na waliofanyiwa upasuaji kubadili jinsia zao (LGBT).

Wajumbe wa Uganda kwenye kikao hicho ni pamoja na Bi. Mourine Osoru  (Wilaya ya Arua), Abdulatif Sebaggala (Kawempe Kaskazini), Bi. Rose Kabagyeni (Wilaya ya Kisoro), Bi. Esther Anyakun  (Wilaya ya Nakapiripirit), Paul Akamba (Busiki) na Francis Mwijukye wa (Buhweju).

Maandamano dhidi ya ushoga na usagaji

Nchi za Afrika na za Kiarabu pamoja na China na Russia zimeunga mkono hoja hiyo ya kupigwa marufuku kikamilifu mijadala kuhusu mashoga na wasagaji katika Bunge hilo kimataifa, huku aghalabu ya nchi za Magharibi zikipinga.

Aghalabu ya nchi za Afrika zimepiga marufuku mahusiano ya watu wenye jinsia moja na haswa ndoa za watu hao wanaojihusisha na liwati na usagaji.