Mufti wa Uganda ataka kupigwa marufuku TikTok nchini humo
Mufti wa Uganda, Sheikh Shaaban Ramadhan Mubajje, ametoa mwito kwa serikali kuu kupiga marufuku programu ya mtandao wa kijamii wa TikTok nchini humo, ambayo anasisitiza kuwa inatumiwa na watu wasio na kazi kuwakashifu na kuwapaka matope watu wengine.
Sheikh Mubajje amesema hayo katika ujumbe wake wa Idul Fitri, ambapo pia ameeleza kusikitishwa na baadhi ya viongozi wa Kiislamu wanaotumia mitandao ya kijamii kutoa taarifa za upotoshaji kwa waumini.
Amesema mtandao wa TikTok ni mbaya zaidi hata kushinda mtandao wa Facebook ambao ulifungwa na serikali huko nyuma, na kwamba wakati umefika wa kuchukuliwa hatua ya ama kupiga marukufu au kuudhibiti mtandao huo.
Mapema mwezi uliopita wa Machi, Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya iliutaka mtandao wa kijamii wa China wa TikTok uondoe maudhui za kingono zinazowalenga na kuwaathiri watoto.
Kwa mujibu wa taarifa ya kiuchunguzi iliyotolewa na mamlaka hiyo, jukwaa la TikTok lilikuwa likipata faida kutokana na maudhui hizo za mambo machafu zenye kuhusisha watoto wenye umri wa miaka 15. Mtandao wa TikTok ndilo jukwaa la tatu kwa kuwa na wafuasi wengi duniani, likitanguliwa na Facebook na WhatsApp.

Wakati huo huo, uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Uganda, umesisitiza kuwa wanafanya kazi kwa mujibu wa katiba ili kumfanya Sheikh Mubajje abakie katika wadhifa wake huo, ingawa ana umri wa miaka 70.
Baadhi ya wanaharakati wa Uganda walienda mahakamani kutaka Sheikh Mubajje alazimishwe kujiuzulu, kwani amehudumu kwenye kiti cha Mufti Mkuu wa Uganda kwa miaka 24, badala ya miaka 10.