Nchi za Ulaya na Asia zataka kuondolewa vikwazo Iran
Nchi za Ulaya na Asia sanjari na kutangaza utayarifu wao wa kuendelea kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya Iran, zimesema kuondolewa vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ni sehemu muhimu ya mapatano hayo ya kimataifa yanayofahamika kama JCPOA.
Katika taarifa ya pamoja baada ya kumalizika Mkutano wa Asia-Ulaya (ASEM) mjini Brussels jana Ijumaa, viongozi wa nchi hizo wamesema makubaliano ya nyuklia ya Iran yanaenda sambamba na matarajio ya madhumuni yake, na kuyaheshimu na kuyatekeleza ni kwa maslahi ya usalama, amani na uthabiti wa dunia.
Siku chache zilizopita, Wizara ya Hazina ya Marekani iliyawekea vikwazo mashirika kadhaa ya Iran zikiwemo benki 20, kwa kisingizio cha kuwa na ushirikiano na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na eti kwa ajili ya kupambana na ugaidi.
Itakumbukwa kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani tarehe 8 mwezi Mei mwaka huu alichukua uamuzi wa upande mmoja wa kuiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya JCPOA; hatua iliyolaaniwa na kupingwa pakubwa ndani ya Marekani na katika uga wa kimataifa.
Baada ya kuchukua hatua hiyo, serikali ya Washington imeanzisha kampeni za kila upande za mashinikizo dhidi ya Iran huku ikitumia kila njia kuzishawishi nchi nyingine ziunge mkono vikwazo vyake vya upande mmoja dhidi ya Tehran.
Trump alisema nchi yoyote itakayoendelea kufanya biashara na Iran kuanzia mwezi Novemba mwaka huu, ijiandae kwa vikwazo na wala haitaruhusiwa kuendelea kufanya biashara na Washington.