Lavrov ataka kuharakishwa uchunguzi kuhusu mauaji ya Khashoggi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza ulazima wa kuharakishwa uchunguzi kuhusu mauaji ya mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia.
Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya Euro-News, Sergei Lavrov ameashiria masuala yanayohusiana na mauaji ya Jamal Khashoggi mwandishi wa habari aliyekuwa akiukosoa utawala wa kifalme wa Saudia na kusisitiza kuwa Moscow inaunga mkono maombi ya kuharakishwa uchunguzi kuhusu mauaji ya mwandishi huyo.
Alexei Pouchkov Mkuu wa Kamisheni ya Siasa ya Baraza la Russia pia amebainisha kuwa kadhia ya mauaji ya Khashoggi yaliyofanywa katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul Uturuki ni mfano wa wazi wa siasa za undumakuwili za Marekani.
Pouchkov ameongeza kuwa serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani inafanya kila iwezalo kustafidi na kila hatua ili kulinda mikataba mikubwa ya uuzaji silaha baina yake na Saudi Arabia hata baada ya mauaji hayo ya kinyama ya Jamal Khashoggi; japokuwa si jambo rahisi kwa Marekani kulinda uhusiano wake na Saudia baada ya kuuliwa mandishi huyo wa habari aliyekuwa akiikosoa Saudia.