UNHCR: Watu milioni 12 duniani hawana utaifa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi , UNHCR limesema kuna watu milioni 12 kote duniani ambao hawana utaifa.
Kwa mintarafu hiyo UNHCR inapigia debe Kampeni ya #I Belong au yaani 'mimi ni wa', ikitimiza miaka minne mwezi huu wa Novemba. Kwa munasaba huo, Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi ametaka serikali zichukue hatua za haraka kuhakikisha ifikapo mwaka 2024 tatizo la watu kutokuwa na utaifa linatokomezwa.
Filippo Grandi ametilia mkazo hoja hiyo wakati huu ambapo idadi ya watu ambao hawana utaifa kote duniani inakadiriwa kuwa milioni 12.
Bwana Grandi ametaka hatua za haraka zichukuliwe kutatua tatizo hilo huku akisisitiza kuwa hatua hizo ni jambo muafaka kufanywa kimaadili, kiutu na kisiasa. Aidha ameongeza kuwa watu wasio na utaifa bado wanakabiliwa na changamoto kupata haki zao za msingi kama vile elimu, matibabu na ajira.
“Ondoeni sheria za kibaguzi ambazo ndio kichocheo cha ukosefu wa utaifa,” amesema Grandi ikieleza kuwa mataifa 25 duniani bado yana vipengele vya ubaguzi wa kijinsia ambavyo vinazuia watoto kupata uraia au utaifa wa mama zao kama ilivyo kwa upande wa baba.
Nchi zilizobadili sheria na kuwapa uraia watu wasio na utaifa ni pamoja na Sierra Leone , Madagascar, Kenya, Kyrgyzstan na Thailand. Mapema mwaka jana serikali ya Kenya iliwakabidihi vitambulisho vya utaifa watu 4000 wa jamii ya wamakonde na kuwafanya kuwa kabila la 43 la Kenya. Watu hao ambao wazazi na babu zao waliwasili nchini Kenya mwaka 1936 kutoka Tanzania na Msumbiji, walikuja kufanya kazi katika mashamba ya mikonge na hawakurudi nchini kwao, na kwa miaka mingi walikuwa wamenyimwa haki zao za msingi za kibinadamu, kwani hawakutambuliwa kama raia wa Kenya.