Iran ina haki ya kurutubuisha tena urani kama jibu kwa Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran ina haki ya kuimarisha urutubishaji urani katika vituo vyake vya nyuklia, kama radiamali kwa hatua ya Marekani ya kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Rai News 24 ya Italia na kuongeza kuwa, "Tuna haki ya kujiondoa JCPOA au hata kuanza kurutubisha tena urani, lakini kuna chaguo jingine. Hata hivyo lazima tudhaminiwe maslahi yetu na nchi za Uaya."
Amesema iwapo Marekani itaachwa iendelee na tabia yake ya kuzishinikiza na kuzidhalilisha nchi za Ulaya, ubeberu huo hautafikia tamati.
Huku akisisitiza haja ya nchi za Umoja wa Ulaya kuchua hatua za kivitendo za kuyanusuru makubaliano hayo, mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amesema 'haiwezekani kuogelea bila kupata unyevunyevu.'
Dakta Zarif amekariri kuwa, mapatano yaliyofikiwa ya JCPOA ni makubaliano mazuri na matunda ya diplomasia na mazungumzo ya miaka mingi, na kwamba Iran haitafanya tena mazungumzo na Marekani kuhusu miradi yake ya nyuklia.
Mnamo Mei 8, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa nchi yake imeondoka katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, ambayo yalifikiwa baina ya Iran na madola sita makubwa duniani, yaani China, Russia, Uingereza, Ufaransa, Marekani pamoja na Ujerumani mwaka 2015; na kutangaza pia kurejesha tena vikwazo dhidi ya Iran, jambo ambalo linaendelea kukosolewa vikali na duru mbalimbali za kimataifa.