Iran na EU zasisitizia haja ya kuendelea kufungamana na JCPOA
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya kwa mara nyingine tena zimesema kuwa pande mbili hizo zitaendelea kuheshimu na kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya Vienna, licha ya Marekani kujiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa.
Hayo yamesemwa katika mkutano baina ya Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran, Dk Ali Akbari Salehi na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, pambizoni mwa Warsha ya Tatu ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Nyuklia baina ya Iran na Umoja wa Ulaya mjini Brussels Ubelgiji.
Dakta Salehi amekariri kuwa, Tehran ina nia ya kweli ya kuendelea kuimarisha na kupanua ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya katika masuala ya nyuklia kwani maendeleo yoyote yatakayopatikana kwenye jambo hilo ni kwa manufaa ya pande mbili na jamii nzima ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mogherini amesema Brussels na Tehran zitaendelea kuwa na ushirikiano wa kistratajia kuhusu shughuli za nyuklia za Iran zenye malengo ya kiraia.
Rais Donald Trump mwezi Mei mwaka huu alitangaza kuindoa Marekani kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, licha ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kutoa ripoti 13 za kuthibitisha kuwa Iran imeheshimu kikamilifu makubaliano hayo.