Mwenyekiti wa Baraza Kuu la UN: Wapalestina wanaendelea kuuawa, kuteseka
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema kuwa, mauaji na mateso ya Wapalestina sasa vimekuwa jambo la kawaida la kila siku lakini inasikitisha kuona kuwa, baadhi ya vyombo vya habari vimepuuza suala hilo.
María Fernanda Espinosa ambaye alikuwa akizungumza kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Wapalestina inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 29 Novemba amesema, watu wa Palestina wanahitajia kuoneshwa mshikamano zaidi kwa sasa kuliko wakati wowote mwingine.
Fernanda Espinosa ameongeza kuwa, hali ya sasa ya watu wa Palestina ni jeraha la kudumu katika dhamira za walimwengu na wanadamu wote wanawajibika kutafuta njia ya kushughulikia kadhia ya Palestina haraka iwezekanavyo.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya kimaisha ya Wapalestina na kusema asilimia 43 ya jamii ya Wapalestina ni wakimbizi na nusu yao wana umri wa chini ya miaka 18.
Tarehe 29 Novemba mwaka 1947 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio lililopelekea kuganywa kidhalimu ardhi ya Palestina katika sehemu mbili za Wapalestina na Wayahudi. Azimio hilo lilikuwa la kidhalimu mno kiasi kwamba, baraza hilo hilo mwaka 1977 lililazimika kuainisha 29 Novemba kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Wapalestina.