Umoja wa Mataifa: Jamii ya kimataifa ina wajibu wa kulinda JCPOA
Kwa mara nyingine tena Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) yanapaswa kulindwa na wadau wote katika eneo na jamii ya kimataifa.
Katika ripoti ya sita kuhusu utekelezwaji wa Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama, Guterres amesisitiza kuwa mapatano hayo ya nyuklia ya Iran ni katika mafanikio makubwa zaidi ya kidiplomasia.
Amesema mambo yasiyo ya msingi na ambayo hayana mafungamano yoyote na JCPOA yanapaswa kushughulikiwa katika anga na mazingira tofauti.
Amefafanua kuwa, "Tunapaswa kuimarisha mafanikio haya makubwa ili kulinda mchakato wa kuzuia kuenea silaha za nyuklia ambao ni msingi wa usalama wa dunia yetu."
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, kulindwa makubaliano ya nyuklia ya Iran ni jambo lenye udharura mkubwa hususan katika kudhamini usalama wa dunia.
Katika ripoti yake miezi sita iliyopita, Guterres alieleza wasiwasi wake juu ya uwezekano wa kusambaratika JCPOA baada ya Marekani kujiondoa kwenye makubaliano hayo, lakini katika ripoti ya mara hii amebainisha kuwa ana wingi wa matumaini kuwa yatabakia hai na yanapaswa kulinda wa nguvu zote.