Makumi wapoteza maisha katika janga la tsunami nchini Indonesia + Video
Makumi ya watu wamefariki dunia na wengine wengi kujeruhiwa kutokana na tsunami iliyosababishwa na mripuko wa volcano nchini Indonesia.
Idara ya Jiolojia nchini humo imesema tsunami hiyo imesababishwa na mawimbi ya chini ya bahari yaliyolikumba Lango Bahari la Sunda, linalounganisha Bahari Hindi na Java, umbali wa kilomita 200 kusini magharibi mwa mji mkuu, Jakarta.
Idara ya Kukabiliana na Majanga imesema watu 170 wameaga dunia huku mamia ya wengine wakijeruhiwa, mbali na makumi ya wengine wakitoweka kutokana na janga hilo la kimaumbile na kwamba maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni Pandeglang katika mkoa wa Banten na mji wa Bandar Lampung, kusini mwa eneo la Sumatra.
Baadhi ya wanasayansi na wanajiolojia wanasema mawimbi hayo ya tsunami yumkini yalisababishwa na mbala mwezi la jana usiku, katika kisiwa cha volcano cha Anak Krakatau.
Oktoba mwaka huu, watu zaidi ya 1,200 walipoteza maisha kutokana na tsunami na mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokikumba kisiwa cha Sulawesi mashariki mwa kisiwa cha Borneo nchini Indonesia; miezi miwili baada ya watu wengine 319 kupoteza maisha kutokana na tetemeko jingine la ardhi katika eneo la Lombok nchini humo.
Inafaa kukumbusha hapa kuwa, mwaka 2004 zilzala ya chini ya maji ilitokea katika Bahari Hindi na kusababisha tsunami katika nchi kadhaa huku Indonesia ikiathiriwa zaidi. Watu 170,000 walifariki dunia kwenye janga hilo la kimaumbile nchini Indonesia hususan katika mkoa wa Aceh.