IFJ: Waandishi habari karibu mia moja wameuawa mwaka 2018 duniani
(last modified Wed, 02 Jan 2019 02:50:10 GMT )
Jan 02, 2019 02:50 UTC
  • IFJ: Waandishi habari karibu mia moja wameuawa mwaka 2018 duniani

Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ) limetangaza kuwa, waandishi habari 94 waliuawa mwaka uliomalizika wa 2018 katika maeneo mbalimbali ya dunia.

Taarifa ya jumuiya hiyo imesema waandishi hao waliuawa ama kwa makusudi, au kutokana na milipuko ya mabomu au kwa kupigwa risasi kwa bahati mbaya wakiwa kwenye maeneo yao ya kazi.

Ripoti ya Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari imemulika zaidi mauaji ya mwandishi habari Msaudi Arabia, Jamal Khashoggi na kuyatambua kuwa ni mfano wa mgogoro unaoendelea kuhusu usalama wa waandishi habari duniani. Khashoggi aliuawa na maafisa wa serikali ya Saudi Arabia akiwa ndani ya ubalozi wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki na mwili wake ukakatwa vipande vipande.

Ripoti hiyo imeashiria kuwa nchi hatari zaidi kwa waandishi habari ni Afghanistan ambako wameuawa waandishi habari 16 kisha Mexico walikouawa waaandishi habari 11, na Yemen imeshika nafasi ya tatu kwa kuwa na waandishi 9 wa habari waliouawa mwaka uliomalizika wa 2018.

IFJ: Waandishi habari karibu 100 waliuawa mwaka jana.

Kwa upande wake Shirika la Wandishi Habari Wasio na Mipaka limesema kuwa waandishi habari 12 waliuawa Yemen pekee mwaka jana na kwamba sita miongoni mwao waliuawa na Saudi Arabia na washirika wake.

Maeneo mengine yaliyoshuhudia mauaji ya waandishi wengi wa habari ni Syria (waandishi wa habari 8) Kisha India (7) na Pakistan, Somalia na Marekani ambako waliuawa waandishi 5 wa habari katika kila mojawapo ya nchi hizo.  

Tags