UNHCR: Vifo vya wahajiri katika Bahari ya Mediterania vimepungua
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50614-unhcr_vifo_vya_wahajiri_katika_bahari_ya_mediterania_vimepungua
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema wahajiri wapatao 2,262 walifariki dunia katika Bahari ya Mediterania mwaka uliomalizika wa 2018, na kwamba idadi ya wahajiri wanaokufa maji katika safari hizo hatarishi imepungua kwa zaidi ya asilimia 25.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jan 03, 2019 11:42 UTC
  • UNHCR: Vifo vya wahajiri katika Bahari ya Mediterania vimepungua

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema wahajiri wapatao 2,262 walifariki dunia katika Bahari ya Mediterania mwaka uliomalizika wa 2018, na kwamba idadi ya wahajiri wanaokufa maji katika safari hizo hatarishi imepungua kwa zaidi ya asilimia 25.

Msemaji wa UNHCR, Celine Schmitt amesema hayo leo mjini Paris nchini Ufaransa na kuongeza kuwa, ingawaje bahari ya Mediterania inasalia kuwa kivuko hatarishi kwa wahajiri na wakimbizi wanaojaribu kuelekea katika nchi za Ulaya, lakini idadi waliokufa maji mwaka jana wakiwa katika safari hizo imepungua, ikilinganishwa na mwaka juzi 2017, ambapo wahajiri 3,139 walipoteza maisha au kutoweka baada ya boti zao kuzama.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri IOM, njia ya majini ya kutoka Libya kuelekea nchi za Ulaya ikiwemo Italia na Malta, ndiyo njia hatari zaidi kwa maafa ya roho za watu inayotumiwa na wahajiri haramu kutoka nchi nyingi hasa za Kiafrika kwa safari za kuelekea barani Ulaya kwa lengo la kutafuta maisha mazuri.

Gadi ya Pwani ya Italia ikiopoa miili ya wahajiri waliokufa maji

Wadadisi wa mambo wanasema mgogoro mkubwa wa wahajiri na wakimbizi unaoshuhudiwa hivi sasa ni matokeo ya siasa za uingiliaji kati za madola ya Magharibi katika nchi za eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika; mgogoro ambao umelihusisha pia bara Ulaya. 

Mwezi uliopita Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat alizikosoa vikali nchi kadhaa za Ulaya zilizokataa kusaini Mkataba wa Kimataifa wa Wahajiri.