Shambulizi la guruneti laua kadhaa msikitini Ufilipino
Kwa akali watu wawili wameuawa katika shambulizi la guruneti lililolenga msikiti mmoja katika eneo la Mindanao kusini mwa Ufilipino.
Kamanda wa polisi katika eneo hilo, Kanali Leonel Nicolas amesema watu wangine wanne wamejeruhiwa katika shambulizi hilo, lililotokea jana alfajiri kabla ya kupambazuko katika mkoa wa Zamboanga ambao wakazi wake wengi ni Wakristo.
Amesisitiza kuwa hujuma hiyo siyo ya ulipizaji kisasi, ikizingatiwa kuwa imetokea siku chache baada ya watu 20 kuuawa katika miripuko ya mabomu katika Kanisa Katoliki katika kisiwa cha Jolo, kaskazini mashariki mwa nchi.
Waislamu walio wachache hususan wanaoishi kusini mwa Ufilipino wamekuwa wakilalamikia ubaguzi na kutengwa, katika taifa hilo ambalo idadi kubwa ya watu wake ni Wakristo wa Kikatoliki.

Julai mwaka jana, Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino alisaini muswada wa sheria inayoruhusu kuundwa eneo jipya lenye mamlaka ya ndani la Waislamu la Bangsamoro, kusini mwa nchi hiyo.
Inaarifiwa kuwa, lengo la serikali kuruhusu kuundwa eneo hilo ni kutamatisha malalamiko ya Waislamu wa maeneo ya kusini mwa nchi, yaliyopelekea kushuhudiwa mgogoro wa kidini na kikaumu kwa karibu nusu karne.