Uturuki: Tunashindwa kuelewa kwa nini Marekani inanyamazia kimya mauaji ya Khashoggi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i51324-uturuki_tunashindwa_kuelewa_kwa_nini_marekani_inanyamazia_kimya_mauaji_ya_khashoggi
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema kuwa, anashindwa kuelewa ni kwa nini Marekani inaendelea kunyamazia kimya mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi, raia wa Saudi Arabia aliyeuliwa kinyama katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo wa mjini Istanbul Uturuki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 04, 2019 04:24 UTC
  • Uturuki: Tunashindwa kuelewa kwa nini Marekani inanyamazia kimya mauaji ya Khashoggi

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema kuwa, anashindwa kuelewa ni kwa nini Marekani inaendelea kunyamazia kimya mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi, raia wa Saudi Arabia aliyeuliwa kinyama katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo wa mjini Istanbul Uturuki.

Amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya serikali ya Uturuki TRT na kuongeza kuwa, kitendo cha Marekani cha kunyamazia kimya mauaji hayo yaliyofanywa na waitifaki wao Saudi Arabia, hakikubaliki kabisa.

"Nashindwa kuielewa kabisa Marekani kwa kimya chake hicho... Tunataka uwazi juu ya kila kitu kwani kilichofanyika katika ubalozi huo mdogo wa Saudia ni mateso na mauaji," amesema.

Mohammad bin Salman ni mtuhumiwa mkuu wa mauaji ya Jamal Khashoggi

 

Siku ya Ijumaa, mshauri wa Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, Yasin Aktay alisema baada ya mkutano wake wa siku ya Ijumaa na timu ya wapalelezi wa Umoja wa Mataifa ambao wako nchini humo kuchunguza mauaji ya Khashoggi yaliyojiri ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul mwezi Oktoba mwaka jana kwamba, timu hiyo inaamini kuwa, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, maarufu kwa jina la MbS, ndie mshukiwa mkuu katika mauaji mwandishi wa habari wa Saudia, Jamal Khashoggi, ambae aliuawa kikatili katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo huko Istanbul Uturuki.

Wakati huo huo Rais Erdogan amesema, kuna wajibu wa kulindwa uoja wa ardhi yote ya Syria na kwamba katika vikao vyote vilivyofanyika baina ya nchi yake na Iran na Russia jambo kuu lililohimizwa ni kulindwa umoja wa ardhi nzima ya Syria.