Misimamo ya Kugongana ya Umoja wa Ulaya kuhusiana na Iran
Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya ikiwa mwanachama wa kundi la 4+1 iliunga mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kukosoa vikali kujiondoa Marekani katika makubaliano hayo muhimu na ya kimataifa.
Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya ulitangaza kuchukua hatua ambazo zitasaidia kuhafifisha taathira hasi za vikwazo vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tadbiri na hatua hizo zinajumuisha kutekelezwa sheria ya kukabiliana na athari mbaya za vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran inayojulikana kama 'Sheria Zuizi' na kuanzisha mfumo wa kifedha unaojulikana kama INSTEX unaokusudia kulinda manufaa ya kiuchumi ya mapatano ya JCPOA kwa maslahi ya Iran.
Pamoja na hayo, taarifa jumla ya Umoja wa Ulaya iliyosambazwa siku ya Jumatatu kuhusiana na Iran ina nukta na mambo yanayogongana ambayo yanatilia shaka na alama ya swali juu ya uratibu wa kimisimamo wa jumuiya hiyo kuhusiana na Iran. Katika taarifa hiyo, Umoja wa Ulaya sambamba na kukaribisha kwa mikono miwili kufungamana kikamilifu Iran na ahadi ilizojifunga nazo kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusisitiza kwamba, kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran ni miongoni mwa nukta za kimsingi katika makubaliano hayo ya nyuklia, umeeleza kusikitishwa kwake pia na hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuiwekea tena vikwazo Iran.
Kimsingi ni kuwa, Umoja wa Uulaya umekiri bayana kwamba, Iran imeheshimu na kutekeleza ahadi zake ilizojifunga nazo kwa mujibu wa makubaliano hayo ya kimataifa ya JCPOA na kwamba, licha ya Marekani kukiuka ahadi na kuiwekea vikwazo Tehran ambavyo havijawahi kushuhudiwa, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bado imeendelea kuheshimu makubaliano hayo.
Licha ya kuwa madola ya Ulaya yaliahidi kwamba, yangechukua hatua za lazima na za haraka ili kufidia hatua za kihasama na kiuadui za Washington, lakini mfumo wa kifedha unaojulikana kama INSTEX unaokusudia kulinda manufaa ya kiuchumi ya mapatano ya JCPOA kwa maslahi ya Iran umeanzishwa baada ya kusuasua kwa miezi kadhaa tena ukiwa na mipaka mingi. Aidha madola ya Ulaya yameshurutisha pia utekelerzwaji wa INSTEX na masuala kama kutekeletwa mfumo wa FATF.
Hamid Baeidinejad, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini London Uingereza anasema: Endapo madola ya Ulaya yatatoa sharti lolote lile, hapana shaka kuwa, Iran haitakubaliani na asili ya kanali hiyo ya kifedha na itachukua hatua inayofaa kuhusiana na mwenendo wote huo.
Katika hali ambayo, Umoja wa Ulaya unatoa taarifa ya kupinga uamuzi wa Marekani kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini iko pamoja na madai mengine ya Washington dhidi ya Iran.
Katika fremu hiyo, Umoja wa Ulaya umeonyesha wasiwasi wake kuhusiana na kuongezeka machafuko katika Mashariki ya Kati na kile ulichokitaja kuwa nafasi ya Iran katika uwanja huo. Aidha Umoja wa Ulaya umedai pia kwamba, Iran imekuwa ikiyasadia kijeshi, kifedha na kisiasa makundi yasiyo ya kiserikali katika nchi za eneo, ikiwemo Syria na Lebanon.
Kadhalika Umoja wa Ulaya umeonyesha wasiwasi wake kuhusiana na mpango wa kiulinzi wa makombora ya Iran na kuutaja kuwa eti unakiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kama ambavyo umeonyesha wasiwasi na kile uliochokitaja kuwa ukiukaji wa haki za binadamu nchini Iran.
Katika taarifa yake hiyo, kiujumla Umoja wa Ulaya umefuata mkondo uleule wa Marekani katika madai yake ambayo hayaakisi ukweli wa mambo kuhusiana na Iran isipokuwa katika kadhia ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Lililowazi ni kuwa, hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuwa mfuasi na mtetezi wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA haitokani na Iran kufungamana na makubaliano hayo, bali chimbuko lake ni maslahi ya Ulaya ambayo inaamini kwamba, kulindwa na kubakishwa makubaliano hayo ni kwa maslahi ya kiusalama ya bara Ulaya.
Hata kama msimamo wa Umoja wa Ulaya katika suala la kulindwa na kuhifadhiwa makubaliano ya nyuklia unahesabiwa kuwa ni jambo chanya, lakini hatua yake ya kuwa pamoja na madai yasiyo na msingi ya Marekani katika uga wa uwezo wa makombora wa Iran pamoja na siasa za Tehran katika Mashariki ya Kati si sahihi hata kidogo.
Madola ya Ulaya yanafahamu vyema kwamba, uwezo wa makombora wa Iran umepanuliwa katika fremu ya kujihami taifa hili na hakuna wakati ambao Tehran ilikuwa muanzishaji wa vita katika eneo hili.
Kiujumla ni kuwa, licha ya kuwa, taarifa jumla ya Umoja wa Ulaya ina nukta kadhaa chanya kama uungaji mkono kwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini ukosoaji na tuhuma zisizo na msingi zilizotajwa katika taarifa hiyo dhidi ya Iran, ni hatua ambayo katu haikubaliwi na Tehran.