Kuendelea mashinikizo dhidi ya mbunge mwanamke Muislamu wa Kongresi ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i51932-kuendelea_mashinikizo_dhidi_ya_mbunge_mwanamke_muislamu_wa_kongresi_ya_marekani
Katika muendelezo wa mashinikizo dhidi ya Ilhan Omar, mbunge Muislamu wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, kwa mara nyingine, wafuasi na waungaji mkono wa Rais Donald Trump wa Marekani wamemtusi mbunge huyo kwa kubandika picha zinazomtambulisha yeye kama gaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 04, 2019 04:07 UTC
  • Kuendelea mashinikizo dhidi ya mbunge mwanamke Muislamu wa Kongresi ya Marekani

Katika muendelezo wa mashinikizo dhidi ya Ilhan Omar, mbunge Muislamu wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, kwa mara nyingine, wafuasi na waungaji mkono wa Rais Donald Trump wa Marekani wamemtusi mbunge huyo kwa kubandika picha zinazomtambulisha yeye kama gaidi.

Katika picha hiyo iliyobandikwa kwenye ukuta wa Baraza la Wawakilishi la jimbo la Virginia Magharibi, Ilhan Omar amefananishwa na magaidi wa shambulio la Septemba 11 mwaka 2001. Kitendo hicho cha chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) kilichofanywa na waungaji mkono wa Trump siku ya Jumamosi kilisababisha watu wawili kujeruhiwa katika fujo na vurumai zilizotokea kwenye hafla ya maadhimisho ya chama cha Republican katika Baraza la Wawakilishi la jimbo la Virginia Magharibi.

Picha inayomtusi na kumnasibisha mbunge Ilhan Omar na shambulio la kigaidi la Septemba 11

Hii si mara ya kwanza kwa mbunge huyo Muislamu kutusiwa na kuvunjiwa heshima. Kabla hajachaguliwa kuwakilisha jimbo la Minnesota katika Kongresi ya Marekani kwa tiketi ya chama cha Democrat, Ilhan Omar alikuwa akijulikana kwa misimamo yake madhubuti dhidi ya Wazayuni; na baada ya kuingia kwenye Baraza la Wawakilishi na kutokana na kubainisha mitazamo yake kwa uhuru, kwa kukosoa siasa za utawala wa Kizayuni pamoja na kuunga mkono kampeni ya kimataifa ya kuususia utawala huo haramu, inayojulikana kwa kifupi kama BDS, amekuwa akiandamwa kila mara na shutuma na lawama za Trump na waungaji mkono wake. Siku ya Jumamosi, Ilhan Omar alieleza kwamba, katika siku za karibuni amepokea jumbe nyingi za vitisho na akawakosoa wanachama wa chama cha Republican kwa kutolaani hujuma hizo zinazomwandama.

Ilhan Omar

Mike Pushkin, mjumbe wa chama cha Democrat katika Baraza la Wawakilishi la jimbo la Virginia Magharibi amelaani hatua hiyo ya wafuasi wa Trump na kueleza kwamba: Harakati hiyo ni ya chuki dhidi ya Uislamu.

Ilhan Omar na Rashida Tlaib, ni wanawake wawili Waislamu waliofanikiwa kuingia kwenye baraza jipya la wawakilishi la Marekani; lakini sambamba na kuanza kuhudumu kama wabunge, si tu hujuma dhidi yao zimeongezeka huku viongozi wengi wa Marekani wakishindwa kuvumilia kauli na misimamo yao, lakini wafuasi na waungaji mkono wa rais wa nchi hiyo Donald Trump, nao pia wamezidisha mashinikizo ya vita vya kinafsi na propganda zinazotokana na chuki zao kwa Uislamu dhidi ya wabunge hao Waislamu.

Baada ya Trump kuingia Ikulu ya White House, harakati za makundi ya mrengo wa kulia yenye misimamo ya kufurutu mpaka na ubaguzi wa rangi nchini Marekani zimeshamiri mno na wakati huo huo Lobi ya Kizayuni ya AIPAC, nayo pia imekuwa na nguvu zaidi ndani ya jamii ya nchi hiyo kutokana na uungaji mkono mkubwa inaopata kwa kiongozi huyo. Kiasi kwamba, msimamo ulioonyeshwa kitambo nyuma na Ilhan Omar dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel uliandamwa na hujuma na shutuma za kila upande za lobi hiyo ya Wazayuni yenye ushawishi mkubwa ndani ya Marekani na kumfanya hatimaye alazimike kuomba radhi.

Ilhan Omar (kushoto) na Rashida Tlaib

Stephen Walt, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Havard ameandika makala katika jarida la Foreign Policy akisema: Njia pekee iliyobaki ili kuzifanya lobi zinazoiunga mkono Israel ziendelee kuwepo ni kuwadunisha na kuwachafulia itibari zao watu wanaoeleza ukweli.

Mtazamo na hatua za chuki dhidi ya Uislamu zinazochukuliwa na Trump, zimezidisha hofu na wasiwasi wa kuongezeka chuki dhidi ya dini hiyo na vitendo vya ukatili na hujuma dhidi ya Waislamu nchini Marekani. Trump na baadhi ya wanasiasa wengine wa Marekani wamejaribu mara kadhaa kutoa kauli za kuinasibisha dini tukufu ya Uislamu na ugaidi.

Trump, ambaye anajulikana kwa sera na misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu

Daniel Benjamin, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Marekani analizungumzia jambo hilo kwa kusema: Badala ya Trump kutoa msaada katika kukabiliana na ugaidi, zaidi amekuwa akichukua hatua zinazopanua wigo wa harakati za magaidi.

Msimamo wa kueneza hofu na chuki dhidi ya Uislamu na kutoa mashinikizo na mbinyo dhidi ya wabunge wanawake Waislamu katika Baraza la Wawakilishi la Marekani unachukuliwa katika hali ambayo, maafisa wa Washington wamekuwa kila mara wakijigamba na kujinasibu kuwa, wao ni vinara wa kutetea uhuru wa kutoa maoni na kujieleza na kudai kwamba Marekani ni nchi pekee ambayo kila mtu anaweza kukosoa na kubainisha imani na itikadi yake kwa uhuru kamili.../