Makumi wakamatwa Marekani kwa kulalamikia mauaji ya kijana mweusi
Makumi ya watu wametiwa mbaroni na polisi ya Marekani kwa kushiriki maandamano ya kupinga hatua ya Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali katika wilaya ya Sacramento jimboni California nchini humo, kuwaondolea mashitaka maafisa wa polisi waliommiminia risasi na kumuua kijana mweusi ambaye hakuwa amejizatiti kwa silaha yoyote mwaka jana.
Vyombo vya habari katika eneo hilo vimeripoti kuwa, maafisa wa polisi walitumia nguvu kupita kiasi kuwakamata waandamanaji hao licha ya kuwa walikuwa wanafanya maandamano ya amani.
Waandamanaji zaidi ya 80 wametiwa mbaroni na maafisa wa polisi ya Marekani kwa kushiriki maandamano hayo ya jana usiku katika mji wa Sacramento jimboni California.
Mwendesha Mashitaka Mkuu wa eneo hilo, Anne Marie Schub Jumamosi iliyopita alitoa taarifa inayohalalisha mauaji ya kijana huyo kwa jina Stephon Clark aliyekuwa na umri wa miaka 22 mnamo Machi mwaka jana.
Mashahidi na mawakili wa kijana huyo aliyeuawa wanasema kuwa Clark alipigwa risasi na maafisa wawili wa polisi wa Sacramento waliyedhani kuwa amebeba bastola, katika hali ambayo alikuwa amebeba simu ya mkononi.
Visa vya ukatili wa polisi wa Marekani dhidi ya raia wa nchi hiyo wenye asili ya Afrika vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara nchini humo.