Sisitizo jipya la Ufaransa la kuheshimu mapatano ya JCPOA
Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ulitiwa saini kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1 mnamo tarehe 14 Julai 2015, na kuanza kutekelezwa rasmi tarehe 16 Januari 2016.
Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya, yaani nchi tatu za Ujerumani, Uingereza na Ufaransa zinayachukulia mapatano hayo kuwa mfano bora unaoweza kuigwa katika utatuzi wa migogoro mingine ya kimataifa. Ni kwa msingi huo ndipo pamoja na kuchukuliwa hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuiondoa nchi yake katika mapatano hayo hapo tarehe 8 Mei mwaka jana, lakini nchi za Ulaya, pamoja na kuwepo shaka nyingi kuhusu utekelezaji wa ahadi zao, zimekuwa zikisisitiza kuendelea kuheshimiwa mapatano hayo, bali zimekuwa zikifanya kila zinaloweza kwa ajili ya kuishawishi Iran iendelee kasalia katika mapatano hayo. Licha ya msimamo huo rasmi wa Umoja wa Ulaya, lakini misimamo ya baadhi ya nchi imepelekea kutiliwa shaka mtazamo halisi wa Troika ya Ulaya ikiwemo Ufaransa juu ya suala hilo. Jumamosi usiku, Gerard Araud, balozi wa Ufaransa nchini Marekani alidai kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba baada ya kumalizika muda wa JCPOA Iran haitaruhusiwa tena kurutubisha madini ya urani. Aliendelea kusema kuwa kupitia mkataba wa kuzuia uenezwaji wa silaha za nyuklia na mkataba mwingine wa ziada, Iran italazimika kuthibitisha kwamba shughuli zake zote za nyuklia ni za amani. Ujumbe wa Twitter wa balozi huyo wa Ufaransa nchini Marekeni uliamsha hasiri ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.
Akijibu madai hayo, Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kupitia ujumbe wa Twitter alionya kwamba iwapo ujumbe wa Gerard Araud utachukuliwa kumaanisha msimamo rasmi wa Ufaransa basi mapatano ya JCPOA na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yatakuwa yamekiukwa na serikali ya Paris. Araqchi aliitaka Ufaransa kuweka wazi mara moja msimamo wake, la sivyo, Iran ichukue hatua za lazima. Matamshi hayo ya balozi wa Ufaransa nchini Marekani yalipelekea Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kumuita siku ya Jumapili na kumlalamikia rasmi Philippe Thiebaud, balozi mpya wa Ufaransa humu nchini, jambo lililopelekea Gerard Araud kufuta katika ukurasa wake wa Twitter madai yake hayo ya kichochezi dhidi ya Iran, na vilevile serikali ya Paris kuchukua hatua ya kuomba rasmi msamaha na kurekebisha msimamo wa balozi wake huyo mjini Washington, kwa kusisitiza kuwa itaendelea kuheshimu na kutekeleza mapatano ya JCPOA.
Huku ikisema kuwa mapatano hayo yalifikiwa na kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia azimio nambari 2231, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imesema kwamba mapatano hayo ni muhimu kwa ajili ya kulinda utulivu na usalama wa dunia.
Iran imekuwa ikizilalamikia mara kwa mara nchi za Umoja wa Ulaya kwa kutotekeleza ahadi zao kuhusiana na mapatano ya JCPOA, ukiwemo mfumo maalumu wa utumaji fedha mashuhuri kama INSTEX na kutaka hatua za dharura zichukuliwe na Troika na vilevile Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kufanikisha jambo hilo. Sasa badala ya nchi za Ulaya kutekeleza ahadi zao kwa ajili ya kuishawishi Iran iendelee kubakia katika mapatano hayo zimekuwa zikifanya mambo ambayo yanaimarisha msimamo haribifu wa Trump dhidi ya mapatano hayo ya kimataifa. Bila shaka msimamo huo wa Ulaya itapelekea tu kudhoofishwa mapatano hayo ambayo wenyewe unakiri kwamba ni muhimu sana katika kuimarisha uthabiti na usalama wa dunia.