Taasisi za Kiislamu za Ufaransa: Imarati na Misri zinawapaka matope Waislamu
(last modified Tue, 23 Apr 2019 03:21:55 GMT )
Apr 23, 2019 03:21 UTC
  • Taasisi za Kiislamu za Ufaransa: Imarati na Misri zinawapaka matope Waislamu

Umoja wa Taasisi za Kiislamu za Ufaransa umesema kuwa, vitendo vya Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri vinaupaka matope Uislamu duniani na kupelekea kuongezeka mashambulizi dhidi ya Waislamu barani Ulaya.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, umoja huo umetoa taarifa maalumu ikilaumu siasa za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Misri na kusema kuwa, vitendo vya kinyama na visivyokubalika ni sawa na kutoa idhini ya kushambuliwa Waislamu, kutengwa na kubandikwa jina la magaidi.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imezungumzia mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea mwezi uliopita katika misikiti miwili ya mji wa Christchurch huko New Zealand na kusema kuwa, matukio hayo ni matunda ya kuongezeka sana chuki zisizokubalika dhidi ya Waislamu huku baadhi ya nchi za Kiarabu zinazoendelea kupiga vita kile zinachodai ni Uislamu wa kisiasa, zikiwa na mchango wa moja kwa moja katika mashambulizi kama hayo.

 

Umoja wa Taasisi za Kiislamu za Ufaransa umesisitizia pia haja ya kuungana Waislamu wa nchi hiyo katika uchaguzi ili kulinda maslahi yao nchini humo.

Kwa mujibu wa umoja huo, idadi ya Waislamu wapiga kura nchini Ufaransa ni watu milioni tano na hii ni katika hali ambayo Waislamu nchini humo wanakabiliwa na changamoto nyingi kubwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka chuki na uchochezi dhidi yao.

Tags