Korea Kaskazini: Marekani irejeshe haraka meli yetu ya mizigo iliyoiiba
(last modified Tue, 14 May 2019 08:08:41 GMT )
May 14, 2019 08:08 UTC
  • Korea Kaskazini: Marekani irejeshe haraka meli yetu ya mizigo iliyoiiba

Korea Kaskazini imeitaja hatua ya Marekani ya kuikamata meli yake ya mizigo kama 'wizi' na kusisitiza kuwa kitendo hicho kinakanyaga roho ya mazungumzo kati ya Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini na Rais Donald Trump wa Marekani yaliyofanyika mwezi Juni mwaka jana.

Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini imesema kuwa, "Marekani imechukua hatua iliyo kinyume cha sheria ya kukamata meli yetu ya mizigo kwa kisingizio cha kufuata maazimio ya vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."

Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini KCNA limemnukuu msemaji wa wizara hiyo akionya kuwa, "Kitendo hicho si tu kinavunja moyo wa mazungumzo ya viongozi wa Pyongyang na Washington, bali pia huo ni ukiukaji wa wazi wa uhuru wetu wa kujitawala."

Hivi karibuni, Kim Jon-un aliipa Marekani hadi mwishoni mwa mwaka huu kubadili mienendo na sera zake dhidi ya nchi hiyo, ili kufanyike duru ya tatu ya mazungumzo. Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini alibainisha kuwa, Washington iko katika hatari ya kurejea kwenye taharuki iliyokuwa nayo huku nyuma, baada ya mkutano wa pili kati yake na Trump kugonga mwamba.

Kim akitazama jaribio la kombora

Mkutano wa pili kati ya Trump na Kim Jong-un wa Korea Kaskazini ulifanyika kati ya tarehe 27 na 28 ya Februari mwaka huu mjini Hanoi, Vietnam ambapo ulimazika bila kufikiwa natija yoyote.

Duru ya kwanza ya mazungumzo ya viongozi hao ilifanyika tarehe 12 Juni mwaka jana nchini Singapore. 

Tags