Utafiti: Aghalabu ya Wamarekani wanapinga kushambuliwa Iran
Utafiti mpya wa maoni unaonesha kuwa akthari ya wananchi wa Marekani hawaungi mkono wazo la kushambuliwa kijeshi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani.
Utafiti huo uliofanywa na shirika la Ipsos kwa ushirikiano na shirika la habari la Reuters umebainisha kuwa, thuluthi mbili ya Wamarekani wanapinga sera za kiuhasama za utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Iran, na wala hawaungi mkono mpango wowote wa kuihujumu kijeshi Jamhuri ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 60 ya wananchi wa Marekani wamesema kuwa Washington haipaswi kuishambulia kwanza Iran, licha ya kuwa asilimia 51 ya waliohojiwa kusema kuwa wanahisi nchi yao itaingia vitani na Iran ndani ya miaka michache ijayo.
Asilimia 49 ya Wamarekani walioshirikishwa katika utafiti huo wa Ipsos hawaridhishwi na namna Trump anavyoishughulikia kadhia ya Iran.
Siasa na hatua za kupenda vita pamoja na vitisho vya Ikulu ya Marekani (White House) zimekuwa zikikabiliwa na radiamali hasi za viongozi wa Marekani na hata serikali za Ulaya.
Aidha viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakisisitiza kuwa watatoa pigo kali kwa hatua yoyote ya kichokozi na ya kupenda vita ya Marekani.