Takht-Ravanchi: Marekani ilikiuka wazi sheria za kimataifa kwa kujiondoa JCPOA
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kujiondoa Marekani katika mpatano ya nyuklia ya JCPOA ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa hasa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Majid Takht-Ravanchi ameyasema hayo katika makala aliyoandika katika gazeti la Washington Post na kuongeza kuwa: "Hata baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia, Iran imeamua kubaki katika mapatano hayo kufuatia ombi la nchi za Ulaya ili izipatie fursa ya kufidia kile ambacho Iran imepoteza kufuatia uamuzi wa upande mmoja wa Marekani wa kukataa kufungamana na ahadi zake."
Takht-Ravanchi ameendelea kusema kuwa, hivi sasa mwaka mmoja baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia, Iran imekuwa ikisubiri nchi za Ulaya zichukue hatua za kivitendo. Ameongeza kuwa, wanachama waliosalia katika JCPOA hasa Umoja wa Ulaya wanapaswa kutekeleza ahadi zao kikamilifu kwa mujibu wa mapatano ya nyuklia na zifidie hasara ambazo Iran imezipata. Amesema hadi sasa hakuna hatua yoyote yenye kuhisika iliyochukuliwa kufidia hasara za kiuchumi ambazo Iran imezipata baada ya Marekani kujiondoa katika JCPOA. Takht-Ravanchi amesema kutokana na hali hiyo kuendelea Iran haina chaguo jingine ila kusimamisha kwa muda utekelezwaji wa baadhi ya ahadi zake katika JCPOA. Nchi zilizosalia katika JCPOA ni zile zinazojulikana kama Kundi la 4+1 linalojumuisha Russia, China, Ufaransa , Uingereza pamoja na Ujerumani na hali kadhalika Umoja wa Ulaya .
Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema sera za Marekani kuhusu Iran hazina muelekeo wa pamoja na kuongeza kuwa: "Si jambo la siri kuwa, baadhi ya wakuu wa Marekani na baadhi ya watawala wa nchi za Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) wanamshinikiza rais wa Marekani ili achukue misimamo mikali dhidi ya Iran.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema kutumwa meli za kivita za Marekani katika Ghuba ya Uajemi ni matokeo ya kutegemea ripoti bandia za kijasusi ambazo zimewasilishwa na wakuu wa Marekani na baadhi ya watawala wa nchi za eneo. Ameongeza kuwa: "Hata wanachama wa Bunge la Kongresi nchini Marekani hawajaunga mkono ripoti hizo bandia."