Russia: Hatua haribifu za nchi za Magharibi nchini Syria hazina natija
(last modified Sun, 09 Jun 2019 03:05:50 GMT )
Jun 09, 2019 03:05 UTC
  • Russia: Hatua haribifu za nchi za Magharibi nchini Syria hazina natija

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa, hatua haribifu za nchi za Magharibi nchini Syria hazina natija yoyote.

Maria Zakharova ameyasema hayo kando ya kongamano la kimataifa la uchumi katika mji wa Saint Petersburg nchini Russia na kuongeza kwamba, ni kwa sababu hiyo ndio maana nchi za Magharibi haziipi tena umuhimu kadhia ya Syria. Amefafanua kwamba sababu kuu ni kwa kuwa nchi hizo zimefeli katika njama zao za kutaka kuiondoa madarakani serikali halali ya Damascus. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameongeza kwamba misimamo ya nchi za Magharibi ya kutaka kumuondoa madarakani Rais Bashar al-Assad wa Syria haina tena faida. Maria Zakharova amesisitiza kwamba baada ya kushindwa magaidi, hivi sasa Wasyria wamepata fursa tulivu na salama ya kujenga mustakabali na maisha mapya, hivyo nchi za Magharibi haziizingatii tena nchi hiyo.

Marekani na washirika wake wanaohusika na uharibifu nchini Syria

Mgogoro wa Syria uliibuka mwaka 2011 baada ya makundi mengi ya kigaidi na ukufurishaji yanayoungwa mkono na Saudia, Marekani na washirika wao, kuivamia nchi hiyo ya Kiarabu kwa lengo la kuleta mabadiliko ya mlingano wa kieneo kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel. Hata hivyo jeshi la Syria kwa kushirikiana na harakati za wananchi na kwa msaada wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran liliweza kusambaratisha njama hizo na kufunga faili la genge la Daesh (ISIS) nchini Syria.