UN: Vita vimewafanya watu milioni 71 duniani kuwa wakimbizi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54213-un_vita_vimewafanya_watu_milioni_71_duniani_kuwa_wakimbizi
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema takriban watu milioni 71 wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na vita na mapigano katika kona mbalimbali za dunia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 19, 2019 07:39 UTC
  • UN: Vita vimewafanya watu milioni 71 duniani kuwa wakimbizi

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema takriban watu milioni 71 wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na vita na mapigano katika kona mbalimbali za dunia.

Ripoti mpya ya UNHCR iliyotolewa jana kwa mnasaba wa Siku ya Wakimbizi Duniani itakayoadhimishwa kesho Alkhamisi imeashiria kuhusu ongezeko la wakimbizi milioni 2 waliofurushwa makwao kutokana na mapigano katika sehemu mbalimbali duniani mwaka jana 2018, ikilinganishwa na mwaka juzi 2017.

Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi amekosoa vikali hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye siku chache zilizopita alitishia kuwa utawala wake utawatimua mamilioni ya wahajiri wanaoishi nchini humo 'kinyume cha sheria'.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya thuluthi mbili ya wakimbizi wote duniani wanatoka katika nchi za Syria, Afghanistan, Sudan Kusini, Myanmar na Somalia.

Wakimbizi wa Kisomali nchini Kenya

Kadhalika mapigano na migogoro imeifanya zaidi ya asilimia 25 ya wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ni kuwa, nchi maskini dunia aghalabu ndizo zinazobeba mzigo wa kuwa wenyeji wa wakimbizi, na wala sio nchi za Magharibi.