Kikao cha Vienna na 'JCPOA'; udharura wa kuwa huru Ulaya kivitendo
(last modified Sat, 29 Jun 2019 06:47:15 GMT )
Jun 29, 2019 06:47 UTC
  • Kikao cha Vienna na 'JCPOA'; udharura wa kuwa huru Ulaya kivitendo

Sambamba na kukaribia kumalizika kwa muhula wa siku 60 uliotolewa na Iran kwa nchi za Ulaya ili zichukue hatua za kivitendo zenye lengo la kulinda mapatano ya nyuklia ya JCPOA, udiplomasia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unafuatilia maslahi yake ya kitaifa bila kujali mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi.

Katika uwanja huo na kabla ya kufanyika kikao cha Ijumaa ya jana cha kamisheni ya pamoja ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA huko Vienna, mji mkuu wa Autria, Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa alisema: "Nchi zilizosalia katika mapatano hayo hazijaweza kufidia madhara na hasara iliyopatikana baafa ya Marekani kujiondoa katika JCPOA." Inafaa kukumbusha kuwa, wakati Rais Donald Trump alipotoa amri ya kuiondoa nchi yake kwenye mapatano ya JCPOA hapo mwezi Mei mwaka jana, nchi za Ulaya ziliwasiliana na Tehran zikiitaka isijiondoe kwenye makubaliano hayo ya kimataifa ambayo ni natija ya mafanikio ya udiplomasia wa kimataifa. Hivi sasa ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja umepita wa subira ya kistratijia ya Iran, udiplomasia na nia njema ya Tehran, lakini nchi za Ulaya zimekuwa zikitoa matamshi matupu ya kuunga mkono mapatano hayo bila kuchukua hatua zozote za kivitendo katika uwanja huo. Muhula wa Iran kwa nchi za Ulaya kwa ajili ya kufidia gharama ya kujiondoa Marekani katika mapatano ya JCPOA umetimia mwaka mmoja, huku Ulaya ikiwa haijaweza kutekeleza ahadi zake kivitendo kwa ajili ya kuyalinda mapatano hayo.

Trump anafanya juu chini kuvunja mapatano hayo yaliyofikiwa kwa juhudi kubwa za udiplomasia wa dunia

Subira ya Iran na kutoa kwake fursa kwa ajili ya kufanikisha juhudi za udiplomasia, bado hakujaweza kuidhaminia maslahi yake ya kitaifa chini ya kivuli cha mapatano hayo, na ni kwa ajili hiyo ndio maana ikaamua kusimamisha kwa muda utekelezaji wa ahadi zake mbili katika mapatano hayo, sambamba na kutimia mwaka mmoja tangu Marekani ijiondoe katika JCPOA. Katika mazingira hayo mashinikizo ya nchi za Ulaya ya kuitaka Iran iendelee kutekeleza ahadi zake za JCPOA, misimamo yao isiyo ya kimantiki na pia upuuzaji wa nchi nyingine za mapatano hayo kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi zao, ni sawa na kukiuka makubaliano ya JCPOA. Katika uwanja huo Alkhamisi iliyopita Majid Takht-Ravanchi, Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa akizungumzia uzembe wa nchi za Ulaya baada ya Marekani kujiondoa JCPOA alisema: "Watu wa Ulaya wamevunja makubaliano, hivyo nchi ambazo ziliahidi kuyatekeleza kikamilifu mapatano hayo zinatakiwa kuchukua hatua za kivitendo." Katika hali hiyo bado hakuonekani juhudi zozote madhubuti zinazofanywa na nchi za Ulaya kwa ajili ya kulinda mapatano hayo. Badala yake nchi hizo zimekuwa zikifuata siasa za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Nchi zilizosalia katika mapatano tajwa zina kibarua kigumu cha ima kutekeleza ahadi na kuyalinda au kuyavunja

Hakuna shaka kwamba katika mazingira hayo Tehran haitaweza kukubali mashinikizo ya Ulaya kwa ajili ya utekelezaji wa upande mmoja wa mapatano hayo ya JCPOA. Katika uwanja huo siku ya Alkhamisi Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alimuandikia barua Bi Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ambapo sambamba na kubainisha uzembe wa nchi za Ulaya katika utekelezaji wa ahadi zao alisema: "Kusimamishwa ahadi zote au baadhi ya ahadi hizo za JCPOA ni haki ya Iran." Hakuna shaka kwamba iwapo nchi za Ulaya kupitia kikao cha Ijumaa ya jana cha kamisheni ya pamoja ya mapatano ya nyuklia hazitachukua hatua za kivitendo, basi tarehe nane Julai mwaka huu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itachukua hatua ya pili ya kupunguza ahadi zake za mapatano ya JCPOA. Hatua yoyote ya utekelezaji ya nchi za Ulaya ikiwemo ya kufungua mfumo maalumu wa mabadilishano ya kibiashara baina ya Ulaya na Iran (INSTEX), ni lazima izingatie kikamilifu maslahi ya kiuchumi ya Iran. Kinyume na hivyo pande zilizosalia katika mapatano tajwa, hususan nchi za Ulaya zitakuwa wabeba dhima wa kufeli au kusambaratika kabisa mapatano hayo ya kimataifa.

Tags