Trump na Netanyahu wabwabwaja baada ya Iran kuongeza urutubishaji wa urani
Hatua ya Iran ya kuingia kwenye awamu ya pili ya kupunguza kiwango cha ahadi zake ndani ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa mujibu wa kifungu nambari 36 cha mapatano hayo, imewatia kiwewe Rais Donald Trump wa Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mike Pompeo na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Mike Pompeo.
Huku akionesha kuingiwa na wahaka mkubwa kufuatia hatua hiyo ya Tehran, Netanyahu amedai kuwa, kitendo cha Iran cha kuongeza kiwango cha urutubishaji wa madini ya urani ni 'hatua hatarishi' na ya taratibu ya Iran kufikia lengo lake la kuunda silaha za nyuklia. Amezitaka Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuliwekea taifa hili vikwazo vikali kama jibu kwa hatua hiyo.
Hii ni katika hali ambayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Javad Zarif amesisitiza kuwa, ni haki ya Tehran kuchukua hatua za kisheria ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA katika kukabiliana na ugaidi wa kiuchumi wa Marekani dhidi yake; na kwamba hatua zote hizo zilizochukuliwa na Iran zitasimamishwa mara baada ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuanza kutekeleza ahadi zao kivitendo.
Kwa upande wake, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amedai kuwa, hatua mpya ya Iran ya kupanua miradi yake ya nyuklia italifanya taifa hili litengwe zaidi na liwekewe vikwazo zaidi. Amedai kuwa Iran haipaswi kuendelea kurutubisha madini yake ya urani. Rais Donald Trump naye ameionya Iran dhidi ya eti kukiuka makubaliano ya JCPOA. Trump amesema, "Wairani wanapaswa kuwa waangalifu kutokana na vitendo vyao."
Hii ni katika hali ambayo, Trump aliyaponda mapatano hayo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita nchini humo, akisisitiza kuwa ndiyo makubaliano mabaya zaidi katika historia, na hata kwenda mbali na kuiondoa nchi yake kwenye mapatano hayo Mei mwaka jana.
Hapo jana Iran ilitangaza kuwa itaendelea kupunguza kiwango cha uwajibikaji wake ndani ya JCPOA kama njia ya kuyalinda mapatano hayo na iwapo baada ya siku 60 nchi za Ulaya zitaendelea kupuuza vipengee hivyo, Tehran itaingia katika awamu ya tatu ya kupunguza ahadi zake ndani ya mapatano hayo ya Vienna.