EU: Iran kupunguza uwajibikaji wake hakujakiuka JCPOA
(last modified Tue, 16 Jul 2019 07:56:54 GMT )
Jul 16, 2019 07:56 UTC
  • EU: Iran kupunguza uwajibikaji wake hakujakiuka JCPOA

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kupunguza uwajibikaji wake katika makubaliano ya nyuklia haijakiuka pakubwa mapatano hayo ya JCPOA.

Federica Mogherini alisema hayo jana Jumatatu mjini Brussels ikiwa imepita wiki moja baada ya Wakala ya Kimataifa ya Nishati ya Nyuklia IAEA kuthibitisha kuwa Tehran imevuka kiwango cha kurutubisha urani kwa asilimia 3.67 kilichoainishwa katika makubaliano ya JCPOA.

Mogherini amekiri kuwa, mapatano hayo ya nyuklia hayako katika hali nzuri hivi sasa lakini anasisitiza kuwa hayajakufa na yanapaswa kulindwa. Amesema Tehran haijaashiria kuwa inataka kutekelezwe kifungu cha JCPOA cha kutatua mgogoro ndani ya mapatano hayo.

Amesema, "JCPOA haiko katika afya nzuri, lakini ingali hai. Tehran inaweza kuangalia upya hatua ilizozichukua. Tunaiomba Iran irejee katika kufungamana kikamilifu na makubaliano hayo."

Tehran: Kuendelea vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na kutowajibika madola ya Ulaya kwa ahadi yalizotoa, yumkini kukaifanya Iran kujiondoa JCPOA

Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif alisema kuwa, endapo madola ya Ulaya yatachukua hatua za lazima kwa ajili ya kutekeleza ahadi na wajibu wao kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA, basi Tehran inaweza kuangalia upya hatua ilizozichukua, vinginevyo Iran itaendelea kupunguza uwajibikaji wake kwenye mapatano hayo kwa mujibu wa kifungo cha 36 cha JCPOA. 

Dakta Zarif alibainisha kuwa, "JCPOA inasalia kuwa makubaliano bora zaidi kwa kadhia hii ya nyuklia ya Iran, na Tehran itaendelea kufungamana na mapatano hayo madhali pande zilizosalia kwayo (Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Russia na China) nazo zitatekeleza wajibu wao.

 

Tags