Aug 16, 2019 03:16 UTC
  • Zarif: Meli ya mafuta ya Iran ilikuwa imezuiwa kinyume cha sheria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekanusha madai ya serikali ya Uingereza kuwa meli ya mafuta ya Iran ya Grace 1 ilikuwa imekiuka sheria za Umoja wa Ulaya kuhusu vikwazo.

Katika ujumbe aliouandika kupitia ukurasa wake wa Twitter Alhamisi usiku, Zarif ameambatanisha nakala mbili za barua ambazo ubalozi wa Iran mjini London umeiandikia Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza na kusema: "Ubalozi wa Iran mjini London umelalamika kuhusu kushikiliwa kinyme cha sheria Meli ya mafuta ya Grace 1 na umeifahamisha Wizara ya Nje ya Uingereza kuwa, vikwazo vya Umoja  wa Ulaya havihusu Iran na huu ni msimamo wa aghalabu ya nchi za Ulaya."

Baada ya Jeshi la Majini la Uingereza kutekeleza uharamia na kuiteka meli ya mafuta ya Iran inayojulikana kama Grace 1 katika eneo la Jabal al Tariq (Gibraltar) mnamo Julai 4, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilikuwa imedai kuwa hatua hiyo ililenga kutekeleza vikwazo vya Umoja wa Ulaya. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa hatua hiyo ya Uingereza ilikuwa kinyume cha sheria.

Hatimaye jana Alhamisi Mahakama ya Jabal al Tariq ilitoa hukumu na kusema meli hiyo ya mafuta ya Iran inachiliwe huru.  Baada ya kuachiliwa huru meli hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imedai kuwa Iran imeahidi kuwa meli hiyo haitaelekea Syria.

Mapema jana pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika ujumbe kupitia Twitter, aliashiria jitihada zilizofeli za Marekani za kutaka wakuu wa Jabal al Tariq waendelee kushikilia Meli ya Mafuta ya Grace 1 na kusema: "Baada ya Marekani kushindwa kufikia malengo yake kupitia ugaidi wa kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuwazuia wagonjwa wa saratani kupata dawa, Marekani ilijaribu kutumia vibaya mfumo wa sheria ili kuiba mali ya Iran baharini."

Jana Ahlamisi, pamoja na kuwepo njama hizo za Marekani ni hatua za serikali ya Uingereza za kuibua taharuki, Mahakama ya Jabal al Tariq iliamuru Meli ya Mafuta ya Iran ya Grace 1 iachiliwe huru.

Uamuzi huo umetajwa kuwa pigo jingine katika sera za Marekani na Uingereza za kukabiliana na Iran.

 

Tags