Aug 16, 2019 10:05 UTC
  • Kuachiliwa meli ya mafuta ya Iran; kushindwa Uingereza na kufedheheka Marekani

Kufuatia diplomasia hai na athirifu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uamuzi wa Mahakama ya Juu ya eneo la Jabal Tariq (Gibraltar), hatimaye meli ya mafuta ya Iran inayojulikana kama Grace 1 imechiliwa na kuruhusiwa kuendelea na safari zake katika maji ya kimataifa.

Licha ya uchochezi na ombi lililotolewa na serikali ya Marekani kwa lengo la kuendelea kushikiliwa meli hiyo ya mafuta ya Iran na hata kuwepo uwezekano wa kuchukuliwa na Marekani, lakini Mahakama ya Juu ya Jabal Tariq imechukua uamuzi wake wa mwisho wa kuiachilia meli hiyo na kuiruhusu iendelee na safari zake za kawaida.

Uamuzi wa mahakama hiyo ni pigo jingine kwa Uingereza sambamba na kufedheheshwa Marekani kwa sababu kutangazwa hadharani katika vyombo vya habari takwa la Marekani la kutaka meli hiyo iendelee kushikiliwa kinyume cha sheria ni jambo ambalo limeiaibisha Marekani katika fikra za waliowengi duniani.

Kuchiliwa huru meli ya Grace 1 kufuatia upinzani wa Iran kuhusiana na masharti yaliyotolewa na serikali ya Uingereza kabla ya kuachiliwa meli hiyo, kwa mara nyingine kunathibitisha mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika medani ya diplomasia na utendaji.

Mbali na hayo, hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Juu ya Jabal Tariq ya kuachilia huru meli ya mafuta ya Iran licha ya kuwepo ombi rasmi la serikali ya Marekani la kutaka kuichukua meli hiyo, inaonyesha wazi kwamba Uingereza bado haiiamini Marekani moja kwa moja na kwamba haiko tayari kuendelea kucheza siku zote katika uwanja wa Washington.

Muhammad Jawad Zarif, mkuu wa diplomasia athirifu iliyopelekea kuachiliwa meli ya Iran

Kutoaminiana nchi mbili hizo kulidhihiri wazi pale Rais Donald Trump wa Marekani alipotangaza hadharani kuwa nchi hiyo haiko tayari kujihatarisha kwa maslahi ya nchi nyingine katika Ghuba ya Uajemi na kuwa Uingereza inapasa kutetea maslahi yake yenyewe katika eneo hilo.

Katika hali hiyo, Uingereza haiko tayari kuendelea kuchochea ghasia na mivutano katika Ghuba ya Uajemi kwa sababu yenyewe kwa sasa inakabiliwa na mgogoro mwingine wa Brexit. Diplomasia athirifu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande mmoja na mvutano wa Uingereza na Umoja wa Ulaya kuhusiana na suala la Brexit kwa upande wa pili, ni mambo ambayo yameilazimisha serikali ya London kuiachilia meli ya mafuta ya Iran.

Katika hali ambayo hatua ya wanamaji wa Uingereza ya kuisimamisha kinyume cha sheria meli ya mafuta ya Iran haikuiletea faida yoyote serikali ya London, hatua ya kisheria ya Iran ya kuisimamisha meli ya mafuta ya Uingereza katika Lango Bahari la Hormuz imezitumia nchi za Magharibi na hasa Uingereza na Marekani ujumbe huu kwamba Iran imeazimia kukabiliana vilivyo na hatua yoyote inayokiuka sheria na wala haikubali mzaha kuhusiana na suala hilo.

Hatua ya kusimamishwa kinyume cha sheria meli ya mafuta ya Iran ni jambo ambalo limekuwa likipingwa vikali na Muhammad Jawad Zarid, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, ambaye Alkhamisi aliandika kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, akijibu taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza kuhusiana na kuheshimiwa vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwamba: Hakuna chochote kilichobadilika na kusimamishwa meli ya mafuta ya Iran ya Grace 1 kulikiuka sheria moja kwa moja.

Serikali ya Uingereza ilidai kwamba meli hiyo ya mafuta ya Iran ilikuwa ikipeleka mafuta nchini Syria na hivyo kukiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya. Hii ni katika hali ambayo kwanza vikwazo hivyo haviihusu Iran na pili tokea mwanzo ilitangazwa wazi kuwa meli hiyo haikuwa ikielekea Syria.

Meli ya mafuta ya Uingereza iliyosimamishwa na Iran kwa kuvunja sheria

Matukio hayo ya meli katika maji ya Jabal Tariq na Lango Bahari la Hormuz yanathibitisha wazi kwamba hatua ya kisiasa na isiyo ya kisheria ya Uingereza inayotekelezwa kwa ushirikiano na uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani, haitaifanya Iran iwache kufuatilia siasa sahihi na za kisheria katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Hatua ya utekaji nyara iliyotekelezwa na Uingereza katika maji ya Jabal Tariq ni ukiukaji wa wazi wa maazimio kadhaa ya kimataifa yanayohusiana na safari za baharini lakini hatua iliyochukuliwa na Iran katika kusimamisha meli ya mafuta ya Uingereza katika maji ya Lango Bahari la Hormuz ilitekelezwa kwa mujibu wa sheria za ubaharia na safari za meli baharini.

Iran ambayo ni nchi muhimu inayolinda usalama wa safari za meli katika Lango Bahari la Hormuz na Ghuba ya Uajemi haukubaki hata kidogo usalama huo na sheria za kimataifa kufanywa kuwa mhanga wa siasa za Uingereza.

Hukumu iliyotolewa jana na Mahakama ya Juu ya Jabal Tariq ya kuachiliwa huru meli ya mafuta ya Iran ya Grace 1 bila shaka ni ushindi mkubwa wa Iran dhidi Uingereza katika mvutano huo wa meli za mafuta.

Tags