Sep 02, 2019 07:42 UTC

Mtandao maarufu wa habari unaotembelewa na watu wengi nchini Ugiriki umetoa ripoti maalumu na kusema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel hauna uwezo wa kukabiliana na wanamapambano wa Kiislamu wa Hizbullah ya Lebanon.

Mtandao huo umesema kuwa, kwa muda wa miaka mingi sasa, Hizbullah ya Lebanon imekuwa ikitekeleza kivitendo kila ahadi inayoitoa na hivi sasa wanajeshi wa Israel wanaishi katika hali ya woga mkubwa.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alitaraji kuwa kwa kuanzisha mashambulizi dhidi ya Hizbullah angeliweza kunufaika kisiasa ndani ya utawala wa Kizayuni, lakini amefeli katika juhudi zake hizo. Matokeo yake ni kwamba uchokozi wa Benjamin Netanyahu dhidi ya Hizbullah ya Lebanon umesababisha hofu kubwa baina ya raia wa utawala wa Kizayuni.

Mashambulizi ya utawala wa Kizayuni kusini mwa Lebanon

 

Jana Jumapili, Hizbullah ya Lebanon ilijibu uchokozi wa Israel kwa kupiga kwa makombora gari la kijeshi la utawala wa Kizayuni na kuangamiza na kujeruhi wanajeshi wote waliokuwemo kwenye gari hilo.

Wakati huo huo Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa majibu yaliyotolewa jana na harakati hiyo ya muqawama wa Kiislamu dhidi ya Israel yameonesha nguvu za taifa la Lebanon na kwamba kama usingelikuwepo ushirikiano baina ya jeshi, muqawama na wananchi, hivi sasa Lebanon isingeliweza kusimama imara kukabiliana na utawala dhalimu wa Israel.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Lebanon, Elias Bou Saab amesema kuwa nchi yake hivi sasa ina nguvu kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote na kwamba itajibu uchokozi wowote utakaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Tags