Trump amuita Rais Sisi wa Misri kuwa dikteta
(last modified Sat, 14 Sep 2019 11:35:31 GMT )
Sep 14, 2019 11:35 UTC
  • Trump amuita Rais Sisi wa Misri kuwa dikteta

Rais Donald Trump wa Marekani ameripotiwa kumtaja Rais Abdul Fattah al-Sisi kuwa dikteta.

Hayo yamefichuliwa na jarida la The Wall Street Journal ambalo limeandika kuwa, Trump alimuita Sisi dikteta mwezi uliopita pambizoni mwa mkutano wa kundi la G7 nchini Ufaransa.

Gazeti hilo limeripoti kuwa, Trump alisikika akiuliza kwa stihizai kwamba,  "Yuko wapi dikteta wangu mpendwa?" pambizoni mwa mkutano wa G7 uliofanyika katika mji wa Biarritz, kusini magharibi mwa Ufaransa. Haijabainika iwapo rais wa Misri aliyasikia matamshi hayo ya kejeli ya Trump au la.

Miongoni mwa maafisa waliokuwapo katika ukumbi palipotokea tukio hilo ni Waziri wa Hazina ya Taifa wa Marekani, Steven Mnuchin, John R. Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani aliyepigwa kalamu nyekundu hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri na Mkuu wa Idara ya Intelijensia ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. 

Trump na Sisi pambizoni mwa mkutano wa G7

Sisi amekuwa akikosolewa kwa kuiongoza Misri kwa mkono wa chuma. Hivi karibuni, Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International liliripoti kuwa, ukandamizaji wa haki ya kujieleza umefikia kileleni katika kipindi cha utawala wa Rais al Sisi. 

Ukandamizaji huo unalenga zaidi wanachama wa harakati ya Ikhwanul Muslimin, waandishi habari, watetezi wa haki za binadamu, wanasheria na hata maafisa wa taasisi za michezo.

Tags