Zarif na Mogherini wajadili njia za kuinusuru JCPOA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Javaad Zarif amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini na wawili hao wamejadili njia za kulinda na kudumisha makubaliano ya JCPOA.
Wawili hao walikutana jana Jumatatu mjini New York pambizoni mwa Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo wametathmini na kubadilishana mawazo juu ya mapatano hayo ya kimataifa.
Dakta Zarif amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katu haitaingia kwenye mapatano mengine kuhusu miradi yake ya nyuklia, iwapo makubaliano ya sasa hayatatekelezwa ipasavyo.
Amesema, "madola hayo ya Ulaya hayajachukua hatua yoyote ya maana ya kutekeleza ahadi zao kwa mujibu wa JCPOA kwa kuwa hawana idhini ya Marekani. Jambo hili limekuwa likionekana wazi tokea Mei 2018."
Kutokana na EU kutofungamana kikamiilifu na mapatano hayo kwa mashinikizo ya Marekani, Septemba 6 Tehran ilianza kutekeleza hatua ya tatu ya kupunguza uwajibikaji wake kwa mujibu wa makubaliano hayo ya nyuklia ya JCPOA.
Mwezi Mei mwaka jana, Rais Donald Trump alichukua hatua ya upande mmoja na kuiondoa Marekani katika makubaliano hayo ya kimataifa yenye baraka kamili za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.