Nchi za Ulaya zatishia kujiondoa kwenye makubaliano ya JCPOA
(last modified Sat, 28 Sep 2019 11:36:37 GMT )
Sep 28, 2019 11:36 UTC
  • Nchi za Ulaya zatishia kujiondoa kwenye makubaliano ya JCPOA

Nchi za Ulaya zimetishia kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA iwapo Iran eti haitafungamana kikamilifu na mapatano hayo.

Viongozi wa nchi za EU wamesema iwapo Iran itachukua hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake kwenye makubaliano hayo mwezi Novemba mwaka huu, basi nchi hizo za Ulaya zitaanza kujiondoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.

Kutokana na EU kutofungamana kikamiilifu na mapatano hayo kwa mashinikizo ya Marekani, Septemba 6 Tehran ilianza kutekeleza hatua ya tatu ya kupunguza uwajibikaji wake kwa mujibu wa makubaliano hayo ya nyuklia ya JCPOA, na hatua ya nne inatazamiwa kuanza kutekelezwa mwezi Novemba.

Mwezi Mei mwaka jana, Rais Donald Trump alichukua hatua ya upande mmoja na kuiondoa Marekani katika makubaliano hayo ya kimataifa yenye baraka kamili za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Donald Trump aliondoa Marekani kwenye JCPOA Mei mwaka jana 2018

Nchi za Ulaya zimekuwa zikishinikizwa na utawala wa Trump zifuate mkondo huo wa Washington wa kujiondoa kwenye mapatano hayo.

Akizungumza mjini New York pambizoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Javad Zarif alisema "madola ya Ulaya hayajachukua hatua yoyote ya maana ya kutekeleza ahadi zao kwa mujibu wa JCPOA kwa kuwa hawana idhini ya Marekani. Jambo hili limekuwa likionekana wazi tokea Mei 2018." 

Tags