Papa azikosoa nchi zinazouza silaha na kuwafukuza wakimbizi
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesema mashindano ya kuuza silaha yanayofanywa na nchi fulani duniani ndiyo sababu ya ghasia na mauaji ya watu wakiwemo watoto wadogo katika nchi zinazoshuhudia vita katika kona mbalimbali duniani.
Papa Francis alisema hayo jana Jumapili katika Medani ya St. Peter’s jijini Vatican, kwa mnasaba wa Siku ya Wahajiri na Wakimbizi Duniani ambayo huadhimishwa na kanisa hilo Septemba 29 kila mwaka.
Amebainisha kuwa, nchi inayozalisha na kuuza silaha inabeba dhima ya mauaji ya watu wasio na hatia, kuvunjika kwa familia, sambamba na kuwepo kwa wimbi la wakimbizi katika kona mbalimbali za dunia.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani amesisitiza kuwa kuna ulazima kwa serikali zote duniani kulinda maisha na utu wa raia wasio na hatia na kudhamini usalama katika kambi za wakimbizi kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Hii si mara ya kwanza kwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis kuzilaumu kwa njia isiyo ya moja kwa moja nchi za Magharibi kutokana na mwenendo wao wa kurundika silaha katika nchi zinazoshuhudia mapigano na vita, na kisha zinakataa kubeba mzigo wa wakimbizi uliosababishwa na vita hivyo.
Aprili mwaka huu, Papa alizihutubu moja kwa moja nchi hizo kwa kusema, "Nchi tajiri; Marekani na Ulaya zinauza silaha zinazotumika kuua watoto na (kuua) watu (wengine) katika maeneo ya vita kama Yemen, Syria, na Afghanistan."