Ripoti: Saudia, DRC na Sudan Kusini zaongoza kwa kuwakandamiza wanawake
Utafiti mpya unaonesha kuwa Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali na Libya ni katika nchi zinazoongoza barani Afrika na duniani kwa ujumla katika kuwakandamiza wanawake.
Utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Wanawake, Amani na Usalama ya Chuo Kikuu cha Georgetown kwa ushirikiano na Kituo cha Utafiti wa Amani cha Oslo umefichua kuwa, Saudi Arabia, Yemen, Afghanistan, Syria, Pakistan na Iraq zimetia fora katika ukandamizaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake.
Utafiti huo umeeleza kuwa, ukandamizaji wa wanawake umepungua kwa kiasi kikubwa katika nchi 60 duniani, lakini dhulma hizo dhidi ya wanawake zimeshtadi katika nchi zinazoshuhudia vita na mapigano.
Katika miaka ya hivi karibuni utawala wa Saudi Arabia umewakamata na kuwatia korokoroni makumi ya wanaharakati wa kike wa kutetea haki za wanawake na kuwatuhumu kuwa wameisaliti nchi, kudhuru maslahi ya taifa na kuwaunga mkono kifedha na kiroho maadui wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa katika nchi 167 duniani tokea mwaka 2017, wanawake bilioni 2.7 wamezuiwa kufanya kazi zinazoonekana kuwa za kiume, huku Saudia ikiongoza katika orodha hiyo ikifuatiwa na Yemen, Sudan, Umoja wa Falme za Kiarabu na Syria.
Aidha utafiti huo wa uliofanywa na Taasisi ya Wanawake, Amani na Usalama ya Chuo Kikuu cha Georgetown kwa ushirikiano na Kituo cha Utafiti wa Amani cha Oslo umeonesha kuwa, Norway, Uswisi, Finland, Denmark, Iceland na Austria zinazongoza kwa kuheshimu haki za wanawake duniani, sambamba na uwepo wa usawa katika nafasi za ajira na mishahara miongoni mwa jinsia zote.