Korea Kaskazini yafanyia majaribio kombora jipya la balestiki
(last modified Fri, 29 Nov 2019 02:36:04 GMT )
Nov 29, 2019 02:36 UTC
  • Korea Kaskazini yafanyia majaribio kombora jipya la balestiki

Jeshi la Korea Kusini limetangaza kwamba Korea Kaskazini imelifanyia majaribio kombora lake jipya la balestiki.

Taarifa iliyotolewa na jeshi la Korea Kusini imethibitisha kuwa nchi hiyo jirani ilifyatua kombora jipya la balestiki mapema jana Alkhamisi. Aidha serikali ya Japan nayo imethibitisha kwamba Pyongyang imelifanyia majaribio kombora jipya ingawa bado haijatoa taarifa zaidi kuhusiana na aina ya kombora hilo lililofanyiwa majaribio. Hiyo ni hatua ya 13 ya majaribio ya makombora kufanyika mwaka huu. Kabla ya hapo pia vyombo vya habari nchini Korea Kaskazini vilitangaza kwamba serikali ya Pyongyang imejiandaa kusonga mbele na hatua zake mpya, iwapo hakutapatikana mafanikio katika udiplomasia pamoja na Washington.

Kiongozi wa Korea Kaskazini akipongeza mafanikio ya majaribio ya jeshi la nchi yake

Taarifa za kufyatuliwa kombora jipya la balestiki la Korea Kaskazini zimejiri katika hali ambayo duru mpya ya mazungumzo kwa ngazi ya wataalamu kati ya Pyongyang na Washington mjini Stockholm, Sweden yalimalizika hivi karibuni bila kufikiwa natija ya maana. Kufuatia kuvunjika mazungumzo hayo, viongozi wa Korea Kaskazini walisisitiza kwamba maadamu Washington haijaachana na hatua zake za uhasama dhidi ya nchi hiyo, basi haitofanya tena mazungumzo na Marekani.

Tags