Russia yafunga maelfu ya tovuti za Intaneti kwa sababu za ugaidi
Serikali ya Russia imetangaza kuwa, tangu kuanza mwaka huu wa 2019 hadi hivi sasa imeshafunga mitandao 50 elfu ya Intaneti kutokana na kueneza taarifa za kigaidi nchini humo.
Shirika la habari la Sputnik limeripoti habari hiyo na kumnukuu Alexander Bortnikov, mkurugenzi wa taasisi ya Huduma za Kiusalama ya Russia (FSB) na kuongeza kuwa, zaidi ya tovuti 50,000 zimefungwa nchini Russia tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2019 kutokana na kueneza propaganda za kigaidi nchini humo.
Bortnikov amesema hayo katika kikao maalumu cha Kamati ya Taifa ya Kupambana na Ugaidi ya Russia na kuongeza kuwa, operesheni za kupambana na ugaidi nchini humo zimepelekea kutiwa mbaroni wanamgambo 241 na waungaji mkono wao 606 katika maeneo tofauti ya Russia.
Mkurugenzi huyo wa taasisi za Huduma za Kiusalama ya Russia (FSB) ameongeza kuwa, juhudi na hatua kubwa za kiusalama zilichokuliwa nchini humo mwaka huu wa 2019 zimesaidia sana kiasi kwamba hakuna tukio lolote la kigaidi lililotokea Russia mwaka huu.
Aidha amesema, maafisa usalama wa Russia wamefanikiwa kuangamiza wanamgambo 32 wakiwemo viongozi tisa wa magenge ya kigaidi na kuwatia mbaroni viongozi wengine 41 wa magenge hayo tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Jukumu la Kamati ya Taifa ya Kupambana na Ugaidi ya Russia ni kuwashirikisha wananchi katika vita hivyo na kushiriki kimataifa katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi duniani.