Korea Kaskazini yafanya 'jaribio jingine muhimu' la kombora
(last modified Sat, 14 Dec 2019 12:27:44 GMT )
Dec 14, 2019 12:27 UTC
  • Korea Kaskazini yafanya 'jaribio jingine muhimu' la kombora

Korea Kaskazini imetangaza kufanya kwa mafanikio 'jaribio jingine muhimu' katika Kituo cha Kurushia Satalaiti cha Sohae siku ya Ijumaa.

Shirika Kuu la Habari la Korea (KCNA) limeripoti kuwa, jaribio hilo ni la 'kutegemewa na la kuzuia hujuma ya nyuklia.'

Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini imesema inashirikiana na Marekani kujaribu kupata maelezo zaidi kuhusu jaribio hilo.

Jaribio hilo la kombora limeripotiwa wakati Disemba 7 Korea Kaskazini pia litangaza kufanya jaribio jingine la kombora ambalo ililitaja kuwa 'muhimu sana.'

Mapema mwezi huu, Korea Kaskazini ilitoa onyo na kusema kuwa  itaitumia Marekani 'zawadi ya Krismasi' na kwamba yaliyomo kwenye kifurishi cha zawadi yatatemgemea matokeo ya mazungumzo baina ya nchi hizo mbili.

Kiongozi wa Korea Kaskazini katika eneo la majaribio ya kijeshi

Korea Kaskazini inapinga vikali uwepo wa majeshi ya Marekani katika Rasi ya Korea na ilikuwa imeipa Washington muhula wa hadi mwisho wa mwaka huu wa 2019 kurejea katika meza ya mazungumzo na iondoe vikwazo dhidi yake la sivyo ijitayarishe kwa chochote kile kinachoweza kutokea.

Hadi sasa Rais Donald Trump wa Marekani na kiongozi wa Korea Kaskazini  Kim Jong Un wamefanya duru tatu za mazungumzo huko Singapore, Vietnam na katika mpaka wa Korea Kaskazini na Korea Kusini. Hata hivyo mazungumzo hayo yalivunjika baada ya Marekani kukataa kutekeleza ahadi ilizotoa kwa Korea Kaskazini katika mazungumzo hayo.

Tags