Iran na China zajadili njia za kuinusuru JCPOA
(last modified Tue, 31 Dec 2019 07:32:58 GMT )
Dec 31, 2019 07:32 UTC
  • Iran na China zajadili njia za kuinusuru JCPOA

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na China wamekutana mjini Beijing na kujadiliana juu ya njia na mikakati ya kuyanusuru makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Mohammad Javad Zarif na Wang Yi wamejadiliana pia kuhusu matukio muhimu ya kieneo na kimataifa. Dakta Zarif amewasili Beijing, mji mkuu wa China leo Jumanne ambapo pia anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wengine wa ngazi za juu wa nchi hiyo kuhusu umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbalimbali.

Mapema jana, Geng Shuang, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema Mohammad Javad Zarif na Wang Yi watagusia pia masuala ya usalama na uthabiti katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Asia Magharibi.

Kabla ya kuelekea China, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran jana Jumatatu alikutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Russia, Sergei Lavrov mjini Moscow ambapo kadhia ya JCPOA ni miongoni mwa masuala yaliyopewa uzito kwenye mazungumzo hayo. 

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na China jijini Beijing

Katika kikao cha pamoja na waandishi wa habari mjini Moscow, Dakta Zarif alisema: "Marekani inataka kuzitwisha nchi zote sera na misimamo yake. Russia na Iran zimekuwa zikipinga mienendo hii kwa kutumia njia mbalimbali kama vile mapatano ya kimataifa ya JCPOA."

Hii ni katika hali ambayo, Iran hivi karibuni ilichukua hatua ya nne ya kupunguza utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya makubaliano ya JCPOA baada ya nchi za Ulaya kushindwa kudhamini maslahi ya Tehran ndani ya makubaliano hayo. 

Tags