Waislamu wa Russia waandamana kulaani mauaji ya Jenerali Soleimani
Waislamu nchini Russia wamefanya maandamano nje ya ubalozi wa Marekani mjini Moscow, kulaani hatua ya ugaidi ya utawala wa Donald Trump wa Marekani ya kumuua shahidi kamanda wa jeshi la Iran, Luteni Jenerali Qassem Soleimani.
Kwa mujibu wa ripota wa shirika la habari la IRNA mjini Moscow, waandamanaji hao ambao walikuwa wametundika picha za Jenerali Soleimani kwenye magari yao wamesikika wakipiga mahoni nje ya ubalozi huo wa Marekani, ambapo wamelaani vikali ugaidi huo wa kiserikali wa Marekani.
Waislamu hao wa Russia wakiwa pamoja na wanaharakati wa kiraia wamelaani vikali hatua ya maafisa wa Ikulu ya Marekani (White House) ya kuruhusu ukatili huo dhidi ya afisa wa serikali, ambapo wametaja ukatili huo dhidi ya Haji Soleimani kama 'mauaji ya kidiplomasia.'
Maandamano kama hayo yameshuhudiwa pia ndani ya siku chache zilizopita katika nchi mbalimbali duniani, zikiwemo Marekani kwenyewe, Uingereza, Yemen, Nigeria na Iraq.
Luteni Jenerali Soleimani aliuawa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi Al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi ya Hashdu Shaabi na shakhsia wanane wengine, katika shambulizi la anga lililotekelezwa na askari magaidi wa Marekani katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mjini Baghdad nchini Iraq alfajiri ya Ijumaa iliyopita.