Umoja wa Ulaya: Hakuna mbadala wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA
(last modified Wed, 15 Jan 2020 02:50:30 GMT )
Jan 15, 2020 02:50 UTC
  • Umoja wa Ulaya: Hakuna mbadala wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA

Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya ametangaza kuwa hakuna mbadala wowote wa mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Josep Borrell Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya alitangaza hayo Jumanne ambapo amethibitisha kupokea barua kutoka 'Troika ya Ulaya' kuhusu kuanzishwa mchakato wa utatuzi wa hitilafu za JCPOA  na kuongeza kuwa: "JCPOA ni mapatano muhimu katika uga wa udiplomasia endelevu wa pande kadhaa na hivyo kuyalinda mapatano hayo sasa kuna umuhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote."

Borrel ameongeza kuwa, yeye kama mratibu wa tume ya pamoja, atasimamia mchakato wa utatuzi wa hitilafu na kwamba mchakato huo unalenga kutatua hitilafu ambazo zimeibuka kuhusu utekelezwaji wa JCPOA katika fremu ya tume ya pamoja.

Aidha Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya amesema mchakato wa utatuzi wa hitilafu unahitaji jitihada kubwa ambazo zinapaswa kuandamana na nia njema ya pande zote.

Nchi tatu za Umoja wa Ulaya yaani Ufaransa, Uingereza na Ujerumani ambazo zinajulikana kama  'Troika ya Ulaya' siku ya Jumanne zilitoa taarifa mjini Brussels na kusema zimeanzisha mchakato wa utatuzi wa hitilafu katika JCPOA.

Pamoja na hayo, wanadiplomasia wa Ulaya wanadai kuwa, lengo la mchakato huo ni kulinda mapatano hayo ya nyuklia kupitia mazungumzo na Iran ili irejee katika utekelezaji wa ahadi zake zote katika JCPOA.

Baada ya Marekani kuchukua uamuzi wa upande mmoja na kujiondoa kwenye mapatano ya JCPOA mwezi Mei 2018, Iran ilijaribu kulinda mapatano hayo kwa sharti kuwa pande zilizoslia zitekeleze ahadi zao lakini kwa muda wa takribani miaka miwili sasa nchi za Ulaya hazijaweza kutekekeleza ahadi zao katika JCPOA hasa kuiwezesha Iran inufaike kiuchumi na mapatano hayo.

Tags